Wednesday, December 5, 2012

Walimu Sekondari Wacheza ‘Table Tennis’ Ofisini Korogwe


Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Bungu wakiwa katika ofisi za walimu 
kuzungumzia mafanikio na changamoto mbalimbali kitaaluma katika shule hiyo.
Ofisi ya Walimu Shule ya Sekondari Bungu.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bungu, Dismas Kimweli (kushoto) akifanya 
mahojiano na Mhariri wa Thehabari.com, Joachim Mushi alipotembelea 
baadhi ya Shule za msingi na sekondari Halmashauri ya Korogwe juzi.

Habari na Thehabari.com na HakiElimu
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Bungu iliyopo Korogwe Vijijini wamelalamikia kitendo cha baadhi ya walimu wao kucheza mchezo wa table tennis ofisini (staff room) tendo ambalo limekuwa likifanyika hata wakati wa kazi/vipindi vya masomo. Malalamiko hayo yametolewa juzi ambapo mwandishi wa Thehabari.com alitembelea shule hiyo kuangalia changamoto mbalimbali za elimu eneo la Korogwe Vijijini.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao kiusalama na mwandishi wa habari hizi baadhi ya wanafunzi hao walisema wapo walimu ambao wamekuwa wakicheza mchezo huo hata wanapokuwa na vipindi jambo ambalo huwakatisha tamaa wanafunzi. “Wapo baadhi ya walimu wamekuwa wakijisahau na kucheza table tennis hata kama ni muda wa vipindi…na endapo akiwaanacheza na kiongozi wa darasa asimfuate kumkumbusha kipindi anaweza asije kabisa,” alisema mmoja wa wanafunzi hao.
Thehabari.com ilifika shuleni hapo na kuingia hadi ofisi ya walimu (staff room) na kushuhudia meza ya table tennis ikiwa imefungwa katikati ya ofisi hiyo tena ikipewa nafasi kubwa zaidi ya vifaa vingine vya kikazi vya walimu hao.
Hata hivyo mwandishi wa habari hizi alipozungumza na Mkuu wa Shule ya Sekondari Bungu,Dismas Kimweli kutaka kujua sababu ya shule hiyo kuweka uwanja wa table tennis ofisini hapo mwalimu huyo alisema wameufunga kwa muda kutokana na kukosa eneo la kuuweka, lakini wanafanya jitihada za kuutoa uwanja huo.
“Ni kweli eneo hili kufungwa uwanja kama huo si sahihi…hili nalielewa lakini tuliufunga kwa muda tu na hivi sasa tunajiandaa kuuamisha,” alisema Kimweli. Akifafanua zaidi alisema kutofundishwa kwa baadhi ya vipindi kwa wanafunzi hakutokani na michezo ya table tennis shuleni bali uchache wa idadi ya walimu shuleni hapo. Alisema kutokana na uchache huo wa walimu baadhi ya mwalimu huwa na vipindi karibia 70 kwa wiki jambo ambalo huwazidi baadhi yao hivyo kujikuta wakitupiwa lawama.
Shule ya Sekondari Bungu iliyoanzishwa mwaka 1989 yenye jumla ya wanafunzi 640 ina walimu 12 tu huku kati ya idadi hiyo walimu watatu kwa wako masomoni.



0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More