HakiElimu ni asasi ya kiraia isiyo ya kibiashara. Imesajiliwa kisheria na wadhamini kama kampuni bila ya mtaji kama ilivyo kwa mujibu wa sheria ya makampuni Tanzania Sura ya 212.
HakiElimu ilianzishwa mwaka 2001 na kikundi cha Watanzania 13 ambao kwa muda mrefu wamekuwa na kiu ya kusimama kwa dhati kutaka kuleta mabadiliko kwa kuboresha elimu kwa watoto wote, hasa kutokana na kuona kwamba hali ya elimu Tanzania ilikuwa katika hali mbaya, na kwamba juhudi za kuleta mabadiliko ya kuiboresha zilionekana kukwama.
Ilionekana wazi kwa kundi hili kwamba hali ya utoaji elimu nchini haujaboreka kama ilivyotarajiwa. Sababu kubwa ni kwamba ufumbuzi uliokuwa ukitolewa ulikuwa wa kisiasa zaidi, na kwamba nyaraka nyingi za kiufundi zilizotolewa na maofisa waliohusika na kazi ya kuleta mabadiliko ya sera hazikukidhi haja kwa sababu hazikuzingatia siasa za mabadiliko ya kimuundo Tanzania.
Wakiwa na wazo hili, waanzilishi wa HakiElimu waliazimia kuunda asasi itakayowawezesha wananchi wa kawaida kushiriki katika kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu. Waliamini hali ya elimu nchini itakuwa bora pindi wananchi wa kawaida watakapohusishwa katika kuleta mabadiliko, kujenga mazingira bora yanayoiwezesha jamii kusimamia kikamilifu suala la elimu. Kwa mantiki hiyo tunaweza kusema HakiElimu inajaribu kuangalia iwapo shule zinaweza kusimamiwa kwa pamoja katika hali ya uwazi na demokrasia, na vilevile kuona iwapo wasio na uwezo (masikini) wanaweza kupata taarifa muhimu zinazoweza kuchangia katika kuleta mabadiliko ya Sera na namna ya utoaji wa elimu.
Wanachama waanzilishi na Bodi ya Wakurugenzi ya HakiElimu inajumuisha watu wa kada mbalimbali; viongozi wa mashirika ya kiraia, vyuo vikuu, vyombo vya habari, asasi za kisheria na taasisi zinazojishughulisha na kazi za utafiti na maendeleo hapa Tanzania. Kwa pamoja wameweza kuleta HakiElimu uzoefu wao wa zaidi ya miaka 20.
Waanzilishi wa HakiElimu.
* Jenerali Ulimwengu: Mwanachama na Mwenyekiti wa zamani wa Bodi ya Wakurugenzi, Mwenyekiti wa zamani wa Habari Corporation; mchambuzi wa mambo mbalimbali ya kijamii, Mwanahabari na pia mchapishaji.
* Elizabeth Missokia: Mwanachama na Mkurugenzi Mtendaji wa sasa wa HakiElimu.
* Rakesh Rajani: Mwanachama na Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa HakiElimu, Mtafiti wa masuala ya Haki za Watoto, Mchambuzi wa Mambo, Mchapishaji na Mwanaharakati.
* Wilbert Kapinga: Mwanachama wa HakiElimu; Mshirika Mkuu, Mkono & Co. na Mlezi wa Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
* Demere Kitunga: Mkurugenzi, E & D Publishers; Mwandishi wa vitabu na Mwanaharakati.
* Elieshi Lema: Mwanachama na Mwenyekiti wa zamani wa Bodi ya Wakurugenzi ya HakiElimu, Mkurugenzi wa E & D Publishers; Mtunzi wa vitabu vya watoto na hadithi.
* Richard Mabala: Mwanachama, HakiElimu; Mshauri wa UNICEF katika masuala ya HIV/AIDS, Mwandishi wa vitabu, Mwanaharakati wa masuala ya Jinsia na Vijana.
* Japhet Makongo: Mwanachama na Meneja wa zamani wa Programu ya Usimamizi wa jamii, Elimu na Mtaalamu wa Maendeleo ya Jamii.
* Marjorie Mbilinyi: Mwanachama na Mjumbe wa zamani wa Bodi ya Wakurugenzi ya HakiElimu; Profesa wa Elimu katika Taasisi ya Taaluma za Maendeleo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; na pia Mratibu wa Mpango wa Usalama wa Chakula Vijijini (Rural Food Security Program).
* Martha Qorro: Mwanachama wa HakiElimu, Mkuu na Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Lugha za Kigeni, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
*Illuminata Tukai: Mwanachama, HakiElimu; Ofisa Mradi wa Elimu, UNICEF Tanzania; Mtetezi wa Haki za Watoto.
* Mary Rusimbi: Mwanachama na Mwenyekiti wa Zamani wa Bodi ya Wakurugenzi ya HakiElimu; na Mwanaharakati wa masuala ya Jinsia.
* Joseph Semboja: Mwanachama, HakiElimu; Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya Research on Poverty Alleviation (REPOA); Mchumi na Mchambuzi wa Sera.
* John Ulanga: Mwanachama, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya HakiElimu; Mkurugenzi Mtendaji, asasi ya Foundation for Civil Society. Pia ni Mtaalamu wa Maendeleo ya Jamii.
* Helen Kijo-Bisimba: Mwanachama, HakiElimu, Mkurugenzi Mtendaji, asasi ya Legal and Human Rights Centre (LHRC). Pia ni Mwanaharakati wa Haki za Binadamu.