Mkakati wa Programu

Kwa ujumla lengo la HakiElimu ni kuhakikisha kwamba kila mtanzania anafurahia fursa ya kupata haki yake ya elimu bora katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari pasipokuwa na ubaguzi wowote. Hii haina maana kwamba mtoto apate alimradi elumu tu, bali iwe ile ambayo itawezesha kukuza utamaduni wa kutekeleza Haki za Binadamu, demokrasia na ushiriki wa wananchi katika masuala mbalimbali yanayowahusu.
Dhana yetu kuhusu shule nzuri ni ile ambayo inakidhi mahitaji ya mtoto, inayozingatia misingi ya jinsia na inayoheshimu haki za watu wote. Ni sehemu ambayo wanafunzi wanapata fursa ya kujifunza na kuwa wabunifu, waweze kujitambua na kupata ujuzi muhimu kwa maisha, wajiheshimu na wajifunze kuheshimu wenzao. Dira hii ndiyo iliyokuwa misingi katika uundwaji wa HakiElimu.
Utendaji kazi wetu unachambua na kushughulikia mambo ambayo yanafanya elimu ishuke ikiwa ni pamoja na suala zima la usimamizi wa utoaji elimu kwa kutoa fursa zaidi ya ushirikishwaji wa umma. Katika zama hizi ambazo uendeshaji wa bajeti unafuata utaratibu wa kisekta (sector-wide approaches), haja ya kuwapo asasi huru zinazowezesha ushiriki mpana wa umma katika kufuatilia utendaji wa serikali ni muhimu kwa demokrasia.
Lengo letu kuu ni kuwawezesha wananchi wa kawaida Tanzania nzima waweze kupata elimu bora ili waweze kujikomboa na kuleta mabadiliko kwanza katika jamii zao, hali kadhalika kuifanya serikali iweze kuwajibika ipasavyo.
Kuna maeneo makuu manne ya kufanikisha kazi hiyo:
·    Kuwawezesha wananchi wajue kinachoendelea,
·    Kuhamasisha mijadala wazi ya kina,
·    Kuwahamasisha wananchi waweze kuchukua hatua, na
·    Kufuatilia na kutathmini mchakato mzima ili kupima kiwango cha serikali inavyochukua hatua kushughulikia maoni na matakwa ya wananchi.
      
Kihistoria, HakiElimu inatambua kwamba mabadiliko makubwa- mathalani; nafasi ya mwanamke katika jamii, mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na utunzaji wa mazingira – yamekuwa yakiletwa na vikundi vya jamii ambapo wananchi wenyewe ndio walikuwa chachu za mabadiliko hayo. Uzoefu wetu unaonyesha kwamba njia ya ushirikishwaji wa umma huleta matokeo mazuri zaidi kuliko kutumia njia ya mikutano ya wadau, vikundi vinavyoshughulikia sera na kuwashawizi washiriki wakuu pekee. Vilevile tumegundua kwamba watoa maamuzi huwa wepesi kuchukua hatua panapokuwa na shinikizo la umma kuliko njia nyengine kama vile kuwepo ushahidi fulani au njia ya matumizi ya hoja pekee.
HakiElimu inawashirikisha wananchi kwa njia ya kuwapa taarifa mbalimbali, midahalo, kufuatilia mchakato na kufanya tafiti hivyo kuwawezesha wananchi, na si HakiElimu waweze kupigania kuleta elimu bora na kuwepo jamii inayofuata misingi ya kidemokrasia. Wananchi wanashirikishwa kikamilifu, na hatua mahsusi zinachukuliwa kwa kuwahusisha wanafunzi-huku mkazo zaidi ukiwekwa kwa wasichana na makundi maalumu ya watu kama vile masikini, wanawake vijijini na walemavu. Tunahamasisha dhana nzima ya watu kuwa na utamaduni wa kuhoji mwenendo wa mambo.
Lengo Kuu
Lengo kuu katika program ya 2008-2011 ni kuwawezesha wananchi wa kawaida Tanzania nzima waweze kupigania kuleta elimu bora kwa ukombozi na kuwepo demokrasia ili waweze kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao kwa kuifanya serikali iwajibike ipasavyo. Kuna maeneo makuu manne ya kufanikisha kazi hiyo:
·    Kuwawezesha wananchi wa kawaida Tanzania nzima wajue kinachoendelea kuhusu elimu kwa ukombozi na demokrasia.
·    Kutakuwa na mijadala wazi ya kina juu ya elimu bora na wajibu wa wananchi.
·    Wananchi Tanzania nzima wataweza kutoa maoni yao na kuchukua hatua kwa kuifanya serikali iwajibike, na kwa njia hii waweze kuleta mabadiliko katika jamii zao.
·    Kwa kupitia yote haya, serikali na taasisi nyingine za umma zitawajibika zaidi katika kushughulikia maoni na matakwa ya wananchi.
      
Vitengo vyote vya program hii huku vikitekeleza kazi zake, vitachangia kuweza kufikiwa lengo hili na matokeo yanayotarajiwa kupatikana.

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More