Thursday, October 20, 2011

Ripoti ya utafiti kuhusu sifa za waalimu kitaaluma, hamasa na moyo wa kufundishaJe, Walimu wetu wana Sifa za Ualimu na Hamasa ya

Kufundisha?

Ripoti ya utafiti kuhusu sifa za waalimu kitaaluma, hamasa na moyo walio nao katika kufundisha na athari zake katika kutoa elimu bora

Oktoba 2011

Shukrani


Utafiti huu ni jitihada za pamoja kati ya HakiElimu na Idara ya Saikolojia ya Elimu na Mafu

nzo ya Mitaala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa

ushirikiano na Wafanyakazi wa HakiElimu Dk. Kitila Mkumbo aliandaa mpango na tafiti pendekezo na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi kuhusu njia za ukusanyaji wa taarifa. Pia alisimamia mchakato mzima wa utafiti na kuandika ripoti kuu.

Wafanyakazi wafuatao walifanya kazi ya utafiti kwa kutembelea maeneo ya utafit


engo la kukusanya data: Elizabeth Missokia, Daniel Luhamo, Charles Mtoi, Robert Mihayo, Glory Mosha, Fausta Musokwa, Naomi Mwakilembe, Edwin Mashasi, Benedicta Mrema, Boniventura Godfrey, Lilyan Omary, Anastazia Rugaba, Frederick Rwehumbiza, Nyanda Shuli, Vicent Mnyanyika na Esther Mashoto.i kwa l

Ripoti hii iliandikwa na Dk. Kitila Mkumbo. Uhariri, tathmini pamoja na ushauri kuhusu ripoti ulitolewa na Elizabeth Missokia, Mtemi Gervas Zombwe, Robert Mihayo na Nyanda Shuli.

Ripoti ya utafiti huu isingefanikiwa bila ya ushirikiano wa wanafunzi, wazazi, wajumbe wa kamati za shule, walimu pamoja na wafanyakazi katika ofisi za wilaya ambao tulifanya nao mahojiano. Tunawashukuru sana kwa michango yao pamoja na utayari wao kufanya kazi nasi.

© HakiElimu 2011,

ISBN: 978-9987-18-019-6

HakiElimu, S.L. P 79401, Dar es Salaam, Tanzania

Simu: (255 22) 2151852/3, Faksi: (255 22) 2152449

Sehemu yoyote ya ripoti hii inaweza kunukuliwa kwa ajili ya matumizi ya elimu na si ya kibiashara, ili mradi tu chanzo kitatajwa na kwamba nakala mbili zitatumwa HakiElimu.

Yaliyomo

Majedwali na Vielelezo. 2

Majedwali 2

Vielelezo. 4

Sehemu ya Kwanza: Usuli wa tatizo la utafiti 5

1.1 Utangulizi 5

1.2 Malengo ya utafiti 7

Sehemu ya Pili: Methodolojia ya utafiti 8

2.1 Mbinu. 8

2.2 Maeneo ya utafiti 8

2.3 Sampuli na washiriki wa utafiti 8

2.4 Zana za kukusanyia data. 9

2.5 Uchambuzi wa data. 9

Sehemu ya Tatu: Matokeo ya utafiti 10

3.1 Matokeo kuhusu miongozo ya taarifa za shule. 10

3.1.1 Taarifa kuhusu shule zilizotafitiwa. 10

3.1.2 Ufaulu wa wanafunzi kitaaluma kwa kuzingatia umiliki wa shule. 12

3.1.3 Uhusiano kati ya sifa za waalimu kitaaluma na ufaulu wa wanafunzi kitaaluma. 13

3.1.4 Tofauti ya ufaulu kwa kigezo cha zana za kufundishia na kujifunzia. 13

3.2 Hamasa na moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu. 14

3.2.1 Taarifa kuhusu waalimu. 14

3.2.2 Ushiriki wa waalimu katika programu za kuendeleza waalimu kitaaluma. 16

3.2.3 Hamasa na mitazamo ya waalimu kuhusu ualimu. 17

3.2.4 Moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu. 20

3.2.5 Kiwango cha moyo wa kujitolea wa waalimu kwa kigezo cha umiliki wa shule. 22

3.2.6 Moyo wa kujitolea na kuridhika na ualimu kwa kigezo cha jinsia. 24

3.2.7 Moyo wa kujitolea na kuridhika na ualimu kwa kuzingatia uzoefu na masomo ya kufundisha 24

3.3 Ufanisi wa uongozi wa shule. 25

3.4 Muhtasari: Uhusiano uliopo baina ya ufaulu wa shule kitaaluma na sifa za waalimu kitaaluma, moyo wao wa kujitolea kwa kazi ya ualimu na maoni yao kuhusu ufanisi wa uongozi wa shule. 27

3.5 Maoni ya waalimu kuhusu kazi ya ualimu: Matokeo ya Majadiliano ya Vikundi 29

3.5.1 Utangulizi 29

3.5.2 Kwa nini waalimu walichagua kazi ya ualimu. 29

3.5.3 Mitazamo ya waalimu kuhusu kazi ya ualimu. 31

3.5.4 Mitazamo ya waalimu kuhusu wanafunzi kufanya vibaya kitaaluma na nini kifanyike kuboresha kiwango cha elimu. 32

4. Muhtasari, Hitimisho na Mapendekezo. 36

4.1Muhtasari 36

4.2 Hitimisho na mapendekezo. 37

Marejeo. 39

Majedwali na Vielelezo

Majedwali

Jedwali 1: Ufaulu wa Wanafunzi Kitaaluma Kulingana na Umiliki wa Shule 12

Jedwali 2: Hamasa na Mitazamo ya Waalimu Kuhusu Kazi ya Ualimu. 18

Jedwali 3: Moyo wa Kujitolea wa Waalimu kwa Kazi ya Ualimu. 20

Jedwali 4: Moyo wa Kujitolea wa Waalimu kwa Masomo Wanayofundisha na Sifa za Kitaaluma 25

Jedwali 5: Asilimia ya Waalimu Waliotathmini Ufanisi wa Uongozi wa Shule Zao. 26

Vielelezo

Kielelezo 1: Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2010. 6

Kielelezo 2: Umiliki wa shule zilizotafitiwa. 11

Kielelezo 3: Kipindi cha kuanzishwa kwa shule zilizotafitiwa. 11

Kielelezo 4: Kipindi cha kuanzishwa kwa shule kulingana na umiliki 11

Kielelezo 5: Ufaulu wa wanafunzi kitaaluma kwa kigezo cha umiliki wa shule 12

Kielelezo 6: Idadi ya waalimu wenye shahada au zaidi kwa kigezo cha umiliki wa shule 13

Kielelezo 7: Idadi ya shule zenye maktaba na maabara kwa kigezo cha umiliki 14

Kielelezo 8: Mgawanyo wa washiriki kulingana na mahali (mkoa) 15

Kielelezo 9: Mgawanyo wa washiriki kulingana na masomo wanayofundisha. 15

Kielelezo 10: Mgawanyo wa washiriki kulingana na sifa za ualimu. 15

Kielelezo 11: Uzoefu wa kazi wa waalimu walioshiriki 16

Kielelezo 12: Idadi ya waalimu walioonyesha kuhudhuria programu za mafunzo kazini katika miaka miwili iliyopita 16

Kielelezo 13: Mambo yaliyowahamasisha waalimu kuchagua kazi ya ualimu. 17

Kielelezo 14: Vigezo vilivyowavutia waalimu kuwa waalimu kwa kuzingatia umiliki wa shule 19

Kielelezo 15: Idadi ya waalimu walioarifu kuwa na moyo wa kujitolea katika vipengele mbalimbali vya kazi ya ualimu 22

Kielelezo 16: Moyo wa kujitolea wa waalimu na kuridhika kwao na shule walizofundisha. 23

Kielelezo 17: Idadi ya waalimu walioarifu kuridhishwa na mazingira ya kazi ya shule zao. 23

Kielelezo 18: Moyo wa kujitolea wa waalimu kwa kigezo cha jinsia. 24

Kielelezo 19: Idadi ya waalimu ‘waliokubaliana sana’ na ‘waliokubaliana’ na kauli kuwa uongozi wa shule yao una ufanisi 27

Sehemu ya Kwanza

Usuli wa hitaji la kufanya utafiti

1.1 Utangulizi

Utoaji wa elimu bora ni jambo muhimu katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Kwa hakika, waandishi wengi wanaona kuwa elimu bora ndiyo njia yenye ufanisi zaidi katika kujenga maadili, mitazamo, tabia na maarifa muhimu kwa watu binafsi ili waweze kutumika kwa manufaa katika jamii iliyotangamana. Kikao cha tatu cha Mkutano Mkuu wa 61 wa Umoja wa Mataifa (GA/SHC/3847) kilisisitiza umuhimu wa elimu bora katika kuleta maendeleo ya jamii, kikitaja kwamba elimu bora ni jambo muhimu sana katika kuleta demokrasia ya kweli na ajira ya kweli. Hali kadhalika, Dira ya Maendeleo ya Taifa (2025) inataja kwamba elimu bora ni muhimu ikiwa taifa litakubali kikamilifu kupambana na changamoto za maendeleo zinazolikabili.

Kuna viashiria kadhaa vya elimu bora. Viashiria viwili kati ya hivyo ni muhimu sana, navyo hutumiwa mara kwa mara katika nchi nyingi. Kiashiria cha kwanza huangalia utendaji wa wanafunzi katika maarifa ya msingi, ambayo ni kusoma, kuandika na kuhesabu. Ripoti iliyotolewa hivi karibuni (Uwezo, 2010) inaonyesha kuwa, ingawa kumekuwa na mafanikio makubwa katika kuandikisha watoto shule, kujenga shule na kutoa mafunzo kwa waalimu, wanafunzi hujifunza maarifa machache mno nchini Tanzania; kiasi kwamba pindi wanapohitimu elimu ya msingi, wanafunzi huwa hawana maarifa ya msingi ya kusoma, kuandika na kuhesabu. Na kiashiria cha pili huangalia matokeo ya mitihani ya taifa.

Nchini Tanzania, mitihani hii ya taifa ni ile inayoandaliwa na kusimamiwa na Baraza la Mitihani la Tanzania. Mitihani ya taifa ni mojawapo ya viashiria vyenye nguvu kuhusu kiwango cha elimu, navyo hutumiwa kufanya maamuzi yahusuyo watu binafsi na taasisi kupitia matokeo ya mitihani. Mitihani ni kiashiria muhimu pia cha kupima watoto wamejifunza kiasi gani, nayo ni chanzo muhimu cha taarifa kwa wazazi pindi wanapofanya maamuzi kuhusu watoto wao. Kwa kutumia kipimo hiki, tunaweza kutoa maoni kwamba kiwango chetu cha elimu kimekuwa kikiporomoka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mathalani, kama Kielelezo 1 kinavyoonyesha, Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2010 yalitikisa nchi nzima baada ya wanafunzi wengi kufeli. Kati ya watahiniwa 354,042 waliofanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2010, watahiniwa 177,021 (sawa na 50%) walipata Daraja la Sifuri, nao watahiniwa 136,633 (38.6%) walipata Daraja la Nne. Watahiniwa 15,335 (4.3%) pekee ndio waliopata Daraja la Kwanza na la Pili, ilihali asilimia 88.6 ya watahiniwa walipata Daraja la Nne na Daraja la Sifuri!

Hivyo basi, kusema kweli, asilimia 88.6 ya watahiniwa walifeli Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2010 kwani hawawezi kuendelea na elimu ya ngazi yoyote ya juu. Athari za kufeli huku ni kubwa mno. Itawawia vigumu mno wanafunzi hawa waliofeli kupata ajira kwani hawana maarifa ya msingi ya kusoma, kuandika na kuhesabu. Pia wanakosa stadi za msingi za maisha kama kujiamini, ubunifu na mbinu za kutatua matatizo.

Kielelezo 1: Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2010. (NECTA 2011)

Sababu kadhaa zimetajwa kuwa chanzo cha hali duni ya elimu hapa nchini. Mosha (2011) ameeleza kwa muhtasari sababu hizo, akiziweka katika makundi makuu mawili, ambayo ni: sababu za kimazingira na sababu za vitendea kazi. Kwa mujibu wa Mosha, sababu za kimazingira hujumuisha mazingira ya kisiasa, kiuchumi, kisheria, kidemografia, kiutamaduni na kimataifa. Sababu za vitendea kazi hujumuisha uongozi duni katika taasisi, ufadhili duni kwa sekta ya elimu, hali duni ya miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, walimu wenye sifa duni na matatizo ya mitaala. Elimu bora imehusishwa pia na utoaji na ustadi wa waalimu (Oduro, Dachi & Fertig, 2008). Oduro na wenzie wamedai kuwa mabadiliko katika elimu barani Afrika yamelenga zaidi kuongeza idadi ya watu wanaopata elimu, huku ubora wa elimu inayotolewa ukipewa umakini mdogo.

Sababu nyingi za kuwepo kwa hali duni ya elimu zilizobainishwa na tafiti zilizotangulia zimekuwa zikizungumzia zaidi kuwepo kwa miundombinu isiyofaa ya kufundishia na kujifunzia. Hususan, kumekuwa na tafiti chache sana ambazo zimelenga kuzungumzia ubora wa waalimu na moyo wao wa kujitolea kama mambo yanayoukilia ujifunzaji wenye ufanisi ambao hatimaye huleta mafanikio kitaaluma. Hakika, uchunguzi wa kina wa programu mbalimbali za zamani na za sasa za kuleta mabadiliko katika elimu zilizoasisiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi unaonyesha, miongoni mwa mambo mengine, kuwepo kwa msisitizo mdogo sana kwa waalimu kama sehemu muhimu katika kuleta mabadiliko katika mfumo wa elimu, hususan linapokuja suala la kuboresha ustawi wao na weledi wao. Kwa mfano, kati ya maeneo 39 ya programu zilizopewa kipaumbele katika Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II), ni programu mbili tu zinazogusia kwa mbali suala la kuboresha ustawi na weledi wa walimu.

Walimu ni sehemu muhimu katika kuleta elimu bora. Elimu bora inahusiana moja kwa moja na ufundishaji bora na ujifunzaji bora. Kuna mambo mengi yanayoukilia ufundishaji bora, miongoni mwayo ni sifa na uzoefu wa waalimu, kiwango cha hamasa waliyo nayo, moyo wa kujituma na hisia za kufundisha na mazingira ya kazi. Tafiti zinaonesha kuwa pindi waalimu wanapokuwa na hamasa na wenye kuipenda kazi ya ualimu, wanafunzi huwa na hamasa ya kujifunza na hujifunza maarifa yanayofundishwa na waalimu wao kwa ufanisi zaidi (Caprara na wenzie, 2006). Hivyo basi, ni muhimu kuwatia hamasa waalimu kama hatua mojawapo ya kushughulikia tatizo la kushuka kwa ubora wa elimu. Kwa sababu hiyo, utafiti huu ulifanywa, kwa upande mmoja, kama hatua ya kujaribu kuondoa pengo hili katika maarifa, na kwa upande mwingine, kuchunguza kwa utaratibu maalumu hatua na mikakati ya kuongeza hamasa na moyo wa kujitolea wa waalimu katika kufundisha.

1.2 Malengo ya Utafiti

Utafiti huu ulilenga kuchunguza jinsi sifa za waalimu kitaaluma na moyo wao wa kujitolea katika kufundisha vinavyoathiri ubora wa elimu kama unavyopimwa kwa kutumia ufaulu wa wanafunzi kitaaluma. Utafiti huu ulilenga zaidi:

· Kutathmini sifa za waalimu kitaaluma katika shule za sekondari za serikali, binafsi na za jamii(kata) na jinsi zinavyohusiana na ufaulu wa wanafunzi kitaaluma

· Kuchunguza utayari na moyo wa kujitolea wa waalimu katika kufundisha na jinsi unavyohusiana na ufaulu wa wanafunzi kitaaluma

· Kubaini maoni ya wadau kuhusu kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika mitihani ya taifa

· Kuchunguza vigezo vinavyotumiwa kuwapangia waalimu masomo ya kufundisha na hamasa na moyo walio nao wa kufundisha masomo hayo

· Kuonyesha maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu namna ya kuboresha elimu nchini Tanzania.

Ripoti hii inaonesha matokeo ya utafiti unaozungumziwa hapa. Ripoti hii ina sehemu kuu nne, nazo ni usuli wa hitaji la utafiti, mbinu za utafiti, matokeo ya utafiti, muhtasari, hitimisho na mapendekezo.

Sehemu ya Pili

Methodolojia ya Utafiti

2.1 Mbinu

Utafiti huu ulishughulikia vipengele kadhaa vya ubora wa elimu. Kwanza, utafiti ulitathimini sifa za walimu kitaaluma katika shule za aina tatu, yaani shule za sekondari za serikali, shule za binafsi na shule za jamii (kata). Pili, utafiti ulichunguza moyo wa kujitolea walio nao waalimu na kuridhika kwao na kazi ya ualimu na jinsi mambo haya yanavyohusiana na ufaulu wa wanafunzi. Kujituma na moyo wa kujitolea wa waalimu ulipimwa kwa kutumia hojaji iliyofanyiwa marekebisho kutokana na zana ambazo zimekuwa zikitumiwa na kuthibitishwa kimataifa, na vilevile kuwashirikisha waalimu katika majadiliano ya vikundi lengwa (imeelezwa chini). Tatu, utafiti ulikusanya kwa mapana maoni ya waalimu kuhusu namna ya kuboresha elimu mashuleni.

Hivyo basi, ni wazi kuwa utafiti huu ulichunguza suala la ubora wa elimu kwa kutumia mitazamo ya waalimu. Utafiti huu ulitumia mbinu mseto na vyanzo mbalimbali vya ukusanyaji data ambazo zilikuwa na msingi wake katika mkabala wa kiidadi na mkabala wa kiubora. Mkabala wa kiidadi ulitumiwa katika kukusanya taarifa za msingi za kiidadi kuhusu demografia ya walimu na alama walizopata kuhusu mitazamo na moyo wa kujitolea walio nao. Mkabala wa kuangalia ubora ulitumiwa kukusanya maoni ya walimu kuhusu kazi ya ualimu, na vilevile maoni yao kuhusu hatua na mikakati ya kuboresha elimu nchini.

2.2 Maeneo ya Utafiti

Utafiti huu ulifanywa katika mikoa sita, ambayo ni Pwani, Mbeya, Kigoma, Singida, Dodoma na Mtwara. Mikoa hii ilichaguliwa kwa makusudi kwa kuzingatia ufaulu wake katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2010, ambapo mikoa miwili ilichaguliwa kutoka kwenye makundi ya mikoa iliyokuwa na ufaulu wa kiwango cha juu, kiwango cha kati, na kiwango cha chini. Mikoa ya Pwani na Mbeya ilikuwa na ufaulu wa kiwango cha juu zaidi, ilhali mikoa ya Kigoma na Singida ilikuwa na ufaulu wa kiwango cha kati, nayo Dodoma na Mtwara ni mikoa iliyokuwa na ufaulu wa kiwango cha chini zaidi.

Katika kila mkoa, shule sita zilichaguliwa kwa makusudi kushiriki katika utafiti huu. Kati ya shule hizi, mbili zilikuwa ni shule kongwe za serikali, ambazo ziliitwa ‘shule za kitaifa za serikali’, mbili zilikuwa ni shule za binafsi na mbili zilikuwa ni shule za jamii, ambazo ziliitwa ‘shule za kata za serikali’. Shule zilichaguliwa kwa kutumia kigezo cha ufaulu wake iwapo ni wa juu au chini na iwapo mahali ilipo shule ni mjini au kijijini.

Kwa faida ya utafiti huu, ‘shule za kitaifa za serikali’ zilitafsiriwa kuwa ni zile shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na serikali ambazo zilianzishwa kuanzia wakati wa uhuru hadi mwaka 2000, kabla ya kuanzishwa kwa programu maalumu ya serikali ya kujenga shule katika kila kata. ‘Shule za kata za serikali’ zinatafsiriwa kuwa ni shule ambazo zimejengwa na wanajamii katika ngazi ya kata kwa msaada wa serikali, ambazo zinamilikiwa na serikali. Hizi ni shule ambazo zimeanzishwa katika miaka ya 2000 kama sehemu ya juhudi za serikali kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari.

2.3 Sampuli ya washiriki wa utafiti

Sampuli ya utafiti ilihusisha zaidi walimu na wakuu wa shule. Walimu walishiriki kwa kujaza hojaji na kushiriki katika usaili/majadiliano ya vikundi lengwa (taarifa zaidi zimetolewa katika kipengele kinachofuata). Sampuli ya waalimu iliteuliwa kwa namna ifaayo kwani waalimu wote waliohudhuria shuleni siku ambayo shule husika ilitembelewa ndio waliombwa kujaza hojaji. Aidha, kati ya walimu sita hadi wanane katika kila shule waliombwa kushiriki katika majadiliano ya kikundi. Hali kadhalika, wakuu wote wa shule na Maafisa elimu wa wilaya zilizoshiriki walisailiwa.

2.4 Zana za kukusanyia data

Zana kuu nne zilitumiwa kukusanya data katika utafiti huu. Kwanza, hojaji ziligawiwa kwa waalimu. Hojaji ya waalimu ilitumiwa kutathmini vipengele vikuu vitano, ambavyo ni: sifa za awali za walimu, mazingira ya kazi, hamasa waliyo nayo waalimu na mitazamo yao kuhusu ufundishaji, moyo wao wa kujitolea kufundisha, na ufanisi wa uongozi wa shule.

Pili, majadiliano ya vikundi lengwa na usaili vilifanywa kwa waalimu na wakuu wa shule. Kwa kiasi kikubwa mambo haya yalilenga kuchunguza sababu za kushuka kwa kiwango cha elimu na maoni na mitazamo kuhusu ufanisi wa walimu na moyo wao wa kujitolea kwa kazi ya ualimu.

Tatu, kulikuwa na mwongozo wa taarifa za shule. Zana hii ilitumiwa kukusanya data za msingi kuhusu shule, ikijumuisha idadi ya walimu na sifa zao kitaaluma, upatikanaji na ubora wa zana za kufundishia na kujifunzia, na ufaulu wa shule katika mitihani ya taifa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

2.5 Uchambuzi wa data

Data za kiidadi kutoka katika hojaji na miongozo ya taarifa za shule iliingizwa katika programu ya kompyuta ya SPSS Toleo la 17.0. Kisha data hizo zilisafishwa na uchambuzi muafaka ulifanywa. Kwa kiasi kikubwa uchambuzi ulihusisha takwimu za kiuelezaji, ingawa uchambuzi wa takwimu unaofikia matokeo kwa kujua sababu zake ulifanywa pia kwa kiwango kidogo.

Usaili na majadiliano ya vikundi lengwa yalirekodiwa neno kwa neno katika vinasa sauti. Usaili na mahojiano haya yalinakiliwa katika maandishi kwa Kiswahili na kutafsiriwa kwa Kiingereza. Mijalada ya lugha zote mbili, Kiswahili na Kiingereza, ilihifadhiwa katika kompyuta na katika diski mwako (flash discs) kama nakala za kumbukumbu. Data za kiubora zilichambuliwa kwa kufuata kiunzi cha uchambuzi wa kimaudhui, ambapo maudhui yalibainishwa na kufafanuliwa kwa kutumia nukuu za washiriki.

Sehemu ya Tatu

Matokeo ya utafiti

Matokeo ya utafiti huu yamewasilishwa katika sehemu kuu nne. Katika sehemu ya kwanza kumewasilishwa matokeo ya utafiti kuhusu miongozo ya taarifa za shule, ambayo yanajumuisha data muhimu kuhusu shule kama vile taarifa kuhusu historia yake, idadi ya walimu na sifa zao kitaaluma, na vilevile ufaulu wa shule katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2010. Aidha, katika sehemu hii kumewasilishwa uhusiano uliopo kati ya sifa za waalimu kitaaluma na ufaulu wa wanafunzi katika mtihani huo wa taifa. Katika sehemu ya pili kumewasilishwa matokeo kuhusu hamasa waliyo nayo walimu na moyo wao wa kujitolea katika kufundisha. Katika sehemu ya tatu kumewasilishwa matokeo kuhusu mitazamo waliyo nayo walimu kuhusu kazi ya ualimu na hatua zipi zichukuliwe kuboresha elimu nchini.

3.1 Matokeo kuhusu miongozo ya taarifa za shule

3.1.1 Taarifa kuhusu shule zilizotafitiwa

Kama ilivyoelezwa awali, jumla ya mikoa sita ilifanyiwa utafiti. Katika kila mkoa, shule sita ziliingizwa katika sampuli ya utafiti, na kufanya jumla yake kuwa shule 36 katika mikoa yote sita. Jumla ya shule 30 zilishiriki kikamilifu katika utafiti (sawa na 83.3%). Hata hivyo, shule 24 tu ndizo zilizojumuishwa katika uchambuzi wa mwisho. Shule zilizobaki ziliondolewa kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ukweli kwamba baadhi ya shule hizo zilikuwa zikitoa elimu ya juu ya sekondari tu (kidato cha tano na sita), ilhali kimsingi utafiti huu ulilenga shule zinazotoa elimu ya awali ya sekondari (kidato cha kwanza hadi cha nne).

Kati ya shule hizo 24, kama Kielelezo 2 kinavyoonyesha, asilimia 29.2 zilikuwa shule za kitaifa za serikali, asilimia 37.5 zilikuwa shule za kata za serikali, asilimia 20.8 zilikuwa shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kikristo, asilimia 4.2 zilikuwa shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu na asilimia 8.3 zilikuwa shule binafsi zinazomilikiwa na watu binafsi.

Idadi kubwa ya shule zilizotafitiwa zilianzishwa kati ya mwaka 1990 na 2000 au baada ya mwaka 2000 (tazama Kielelezo 3). Kama ilivyotarajiwa, na kama inavyooneshwa katika Kielelezo 4, idadi kubwa (85.7%) ya shule za kitaifa za serikali zilizotafitiwa zilianzishwa kabla ya miaka ya 1990, wakati idadi kubwa (88.9%) ya shule za kata za serikali zilizotafitiwa zilianzishwa baada ya mwaka 2000. Idadi kubwa (60%) ya shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kikristo na Kiislamu zilianzishwa kati ya mwaka 1990 na 2000, ilhali idadi kubwa ya shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za watu binafsi zilianzishwa kabla ya mwaka 2000. Hii inaashiria kuwa, katika miaka ya karibuni, serikali, kupitia juhudi mbalimbali za wanajamii, imekuwa mwanzilishi mkuu wa shule za sekondari nchini.

Kielelezo 2: Umiliki wa shule zilizotafitiwa (Jumla = 24)

Kielelezo 3: Kipindi cha kuanzishwa kwa shule zilizotafitiwa

Kielelezo 4: Kipindi cha kuanzishwa kwa shule kulingana na umiliki

3.1.2 Ufaulu wa wanafunzi kitaaluma kwa kuzingatia umiliki wa shule

Uchambuzi ulifanywa kuchunguza ufaulu wa wanafunzi kitaaluma kwa kuzingatia umiliki wa shule. Ufaulu wa shule kitaaluma ulichunguzwa kwa kuzingatia Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2010 ya shule husika. Matokeo hayo yameoneshwa kwa muhtasari katika Jedwali 1 na katika Kielelezo 5.

Pindi matokeo haya yalipochambuliwa kwa kuzingatia kigezo cha umiliki, yalionyesha kuwa shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kikristo zilifaulu kwa kiwango cha juu sana kuliko zile zinazomilikiwa na asasi nyingine. Kadhalika, kama ilivyotarajiwa, kwa ujumla, shule za kata za serikali zilifanya vibaya sana katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2010. Mathalani, asilimia 65 ya watahiniwa katika shule za kata za serikali walipata Daraja la Sifuri, huku asilimia 29.3 wakipata Daraja la Nne na asilimia 5.2 tu wakipata kati ya Daraja la Kwanza na Daraja la Tatu.

Jedwali 1: Ufaulu wa Wanafunzi Kitaaluma Kulingana na Umiliki wa Shule[1]

Daraja

Serikali-Kitaifa

Serikali-Kata

Binafsi-Kikristo

Watu- Binafsi

Daraja la I & II

13.8

1.2

71.9

2.9

Daraja la III

15.7

4

5

14.5

Daraja la IV

37.5

29.3

13.7

66.7

Daraja la 0

33.0

65.5

9.4

15.9

Kielelezo 5: Ufaulu wa wanafunzi kitaaluma kwa kigezo cha umiliki wa shule

3.1.3 Uhusiano kati ya sifa za walimu kitaaluma na ufaulu wa wanafunzi kitaaluma

Sifa za waalimu kitaaluma zilipimwa katika viwango vinne. Shule ambayo asilimia 80-100 ya waalimu wake walikuwa na shahada ilichukuliwa kuwa na ‘sifa bora’, ilhali shule ambayo asilimia 50-79 ya waalimu wake walikuwa na shahada ilichukuliwa kuwa na ‘sifa nzuri’. Shule ambayo asilimia 40-49 ya waalimu wake walikuwa na shahada ilichukuliwa kuwa na ‘sifa ya wastani’. Nayo shule ambayo pungufu ya asilimia 40 ya waalimu wake walikuwa na shahada ilichukuliwa kuwa na ‘sifa duni’.

Kama Kielelezo 7 kinavyoonyesha, shule za kitaifa za serikali zilikuwa na idadi kubwa zaidi ya waalimu wenye sifa nzuri kitaaluma, zikifuatiwa na shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kikristo. Shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu na watu binafsi zilikuwa na idadi ndogo zaidi za waalimu wenye sifa nzuri kitaaluma. Mathalani, wakati asilimia 85.7 ya waalimu katika shule za kitaifa za serikali zilizotafitiwa na asilimia 40 ya waalimu katika shule binafsi zilizotafitiwa zinazomilikiwa na asasi za Kikristo walikuwa na shahada, hakukuwa na mwalimu hata mmoja aliyekuwa na shahada katika shule binafsi zilizotafitiwa zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu.

Hata hivyo, ikumbukwe kwamba, kati ya waalimu 303 waliotafitiwa, waalimu 11 (3.6%) tu ndio waliotoka katika shule zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu, waalimu 21 (6.9%) tu ndio waliotoka katika shule zinazomilikiwa na asasi za Kikristo, na waalimu 39 (12.9%) tu ndio waliotoka katika shule zinazomilikiwa na asasi za watu binafsi. Waalimu walio wengi walitoka katika shule za kitaifa za serikali (116) na shule za kata za serikali (116).

Kielelezo 6: Idadi ya waalimu wenye shahada au zaidi kwa kigezo cha umiliki wa shule

3.1.4 Tofauti ya ufaulu kwa kigezo cha zana za kufundishia na kujifunzia

Katika kipengele hiki, zana kuu mbili za kufundishia na kujifunzia ziliangaliwa, nazo ni maabara na maktaba. Kwa mujibu wa sera ya taifa, kila shule ya sekondari inapaswa kuwa na maabara tatu – moja kwa somo la fizikia, moja kwa kemia, na moja kwa biolojia. Hata hivyo, shule chache tu ndizo zilizokuwa na maabara zote tatu. Kwa sababu hiyo, kigezo kikuu cha uchambuzi na ulinganishi kilikuwa ni kuwepo kwa maabara walau moja na maktaba. Kama Kielelezo 6 kinavyoonyesha, shule za kitaifa za serikali na shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kikristo pekee ndizo zilizokuwa na maabara walau moja na maktaba.

Kulikuwa na tofauti kubwa kitakwimu katika ufaulu wa wanafunzi kitaaluma kati ya shule zilizokuwa na maabara (X2= [N=24, 4] =18.80, p=.001, Phi=.89) na maktaba (X2= [N=24, 8] =21.38, p=.006, Phi=.94) na zile ambazo hazikuwa nazo, hali iliyoashiria kuwa vigezo hivi viwili vilikuwa muhimu kwa ufaulu wa wanafunzi kitaaluma.

Kielelezo 7: Idadi ya shule zenye maktaba na maabara kwa kigezo cha umiliki[2]

3.2 Hamasa na moyo wa kujitolea walio nao walimu kwa kazi ya ualimu

3.2.1 Taarifa kuhusu waalimu

Jumla ya waalimu 303 walijaza hojaji. Kati yao, asilimia 70.5 walikuwa wanaume na asilimia 29.5 walikuwa wanawake. Umri wao wa wastani ulikuwa miaka 33.0 (Achano Kuu (SD)=9.2), nao ulianzia miaka 19 hadi 67.

Kulikuwa na mgawanyo sawa wa washiriki katika mikoa yote iliyoshiriki, ingawa kulikuwa na idadi ya juu kidogo ya washiriki kutoka mkoa wa Pwani (tazama Kielelezo 8). Idadi kubwa (40%) ya waalimu waliojaza hojaji walikuwa waalimu wa masomo ya Sanaa na Sayansi za Jamii, kulinganisha na waalimu wa Sayansi na Hisabati (37%) na waalimu wa Lugha (23%) (tazama Kielelezo 9).

Waalimu walio wengi ama walikuwa na stashahada (38%) au shahada (42%) ya elimu (Kielelezo 10). Zaidi ya hayo, kama Kielelezo 10 kinavyoonyesha, waalimu wengi waliojaza hojaji walikuwa na uzoefu wa kufundisha usiozidi miaka mitano.

Kielelezo 8: Mgawanyo wa washiriki kulingana na mahali (mkoa)

Kielelezo 9: Mgawanyo wa washiriki kulingana na masomo wanayofundisha

Kielelezo 10: Mgawanyo wa washiriki kulingana na sifa za ualimu

Kielelezo 11: Uzoefu wa kazi wa waalimu walioshiriki

3.2.2 Ushiriki wa waalimu katika programu za kuendeleza waalimu

Ili kuchunguza ushiriki wao katika programu za kuendeleza waalimu, waalimu waliombwa kuonyesha iwapo walipata kuhudhuria mafunzo yoyote ya ualimu/programu zozote za kujiendeleza wakiwa kazini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Matokeo yanaonesha kuwa asilimia 15.3 tu ya waalimu ndio walioonyesha kuwa walipata kushiriki katika programu fulani ya kujiendeleza kitaaluma katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Majibu yaliyotolewa na waalimu wote, pasipo kuzingatia umiliki wa shule zao, yalielekea kufanana kwa kiasi fulani, ingawa idadi kubwa kidogo ya waalimu wa shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kikristo walionesha kuwa walipata kuhudhuria programu za kujiendeleza kitaaluma kuliko waalimu wa shule nyingine (Kielelezo 12).

Kielelezo 12: Idadi ya waalimu walioonyesha kuhudhuria programu za mafunzo kazini katika miaka miwili iliyopita[3]

3.2.3 Hamasa na mitazamo ya walimu kuhusu ualimu

Katika kuchunguza hamasa na mitazamo waliyo nayo kuhusu ualimu, waalimu walipewa vifungu 19 vya maelezo na kuombwa kutoa maoni yao kwa kuchagua jibu mojawapo kati ya majibu ya aina tano yaliyoanzia na ‘ninakubaliana sana’ hadi ‘sikubaliani kabisa’. Jedwali 3 linaeleza kwa muhtasari matokeo hayo. Uchunguzi wa makini wa matokeo hayo ulionyesha kuwepo sababu kuu nne kwa nini walimu wanaweza kuchagua kazi ya ualimu na kuendelea nayo. Sababu hizo ni kama vile ‘ni rahisi kupata ajira’, ‘kwa sababu ualimu hutoa fursa zaidi za kujiendeleza kielimu’, ‘shauku ya kusaidia wengine’ na ‘shauku ya kufundisha somo/masomo niyapendayo’. Zaidi ya asilimia 60 ya waalimu ama ‘walikubaliana sana’ au ‘walikubaliana’ na maelezo haya.

Uchambuzi wa vigezo ulifanywa kwa kuchunguza muundo wa ndani wa vifungu hivi 19 vya maelezo kwa lengo la kubainisha vigezo vikuu vinavyowahamasisha waalimu kuchagua kazi ya ualimu. Vigezo vikuu vitatu vilijitokeza, navyo ni shauku na moyo wa kupenda kusaidia wengine, kuvutiwa na watu wengine mashuhuri, na mazingira mazuri ya kazi. Matokeo yanaonesha kuwa ‘shauku na moyo wa kupenda kusaidia wengine’ ndicho kigezo kikuu kinachoweza kuwahamasisha walimu kuchagua kazi ya ualimu, ambapo asilimia 45 ya washiriki walichagua kipengele hiki kuwa ndiyo sababu kuu iliyowafanya kuchagua na kuendelea kufanya kazi ya ualimu. Kulikuwa na vifungu vikuu vinne vya maelezo katika kipengele hiki. Vifungu hivyo ni ‘shauku ya kusaidia watu wengine’, ‘moyo wa kupenda kufanya kazi na watoto’, ‘shauku ya kufundisha somo/masomo niyapendayo’ na ‘inaendana na haiba yangu’.

Kuvutiwa na watu wengine mashuhuri ni kigezo kilichoonesha kuwa huwahamasisha waalimu wachache zaidi kuchagua kazi ya ualimu, ambapo asilimia 11.4 tu ya washiriki ndio walioonesha kuwa hii ndiyo sababu iliyowafanya kuchagua kazi hii. Asilimia 16 tu ya waalimu walioshiriki walichagua kazi ya ualimu kwa sababu kuna ‘mazingira mazuri ya kazi’ (tazama Kielelezo 13).

Kielelezo 13: Mambo yaliyowahamasisha waalimu kuchagua kazi ya ualimu

Jedwali 2: Hamasa na Mitazamo ya Waalimu Kuhusu Kazi ya Ualimu

% (N=)

Maelezo

Ninakubaliana Sana

Ninakubaliana

Sikubali Wala Sikatai

Sikubaliani

Sikubaliani Kabisa

SA+A

SD+D

1. Ni rahisi kupata ajira

28.7

31.4

19.8

10.2

7.6

60.1

17.8

2. Ndiyo kazi pekee niwezayo kuipata kwa sifa nilizo nazo kitaaluma

8.6

20.8

12.2

34.3

21.1

29.4

55.4

3. Kazi ya ualimu inanipa uhakika wa ajira

14.9

25.7

21.5

20.1

14.2

40.6

34.3

4. Kuna mshahara mkubwa

1.7

3.3

11.9

26.1

53.5

5

79.6

5. Kuna mazingira mazuri ya kazi

5.0

16.8

21.8

26.1

27.1

21.8

53.2

6. Inakupa hadhi kubwa katika jamii

4

17.5

20.8

28.4

24.1

21.5

52.5

7. Ualimu unanipa matazamio mazuri ya kupata kazi

8.6

29.7

21.1

18.8

16.5

38.3

35.3

8. Kwa kuwa ualimu hunipa fursa zaidi za kujiendeleza kielimu

23.8

37

14.9

9.6

10.9

60.8

20.5

9. Kwa kuwa serikali inajali elimu

9.6

19.8

26.1

24.1

15.8

29.4

39.9

10. Moyo wa kupenda kufanya kazi na watoto/vijana wadogo

11.6

29.4

16.8

20.1

17.5

41

37.6

11. Inaendana na haiba yangu

13.2

27.7

25.7

15.5

13.2

40.9

28.7

12. Shauku ya kusaidia watu wengine

30.7

37.3

13.5

7.9

7.6

68

15.5

13. Shauku ya kufundisha masomo niyapendayo

27.1

37

13.5

9.9

9.6

64.1

19.5

14. Kuvutiwa na waalimu mashuhuri

6.6

19.1

21.5

29.7

18.8

25.7

48.5

15. Kuvutiwa na wanafamilia

5.9

16.8

22.1

29.7

21.5

22.7

51.2

16. Kuvutiwa na wanarika wenzangu

3.3

12.5

19.5

33.7

27.1

15.8

60.8

17. Kuvutiwa na vyombo vya habari

4.3

9.6

16.8

35

30.4

13.9

65.4

18. Kuakisi imani yangu ya kidini

7.6

15.2

16.8

28.4

27.4

22.8

55.8

19. Ugumu wa kupata ajira

10.9

22.8

24.4

18.2

20.1

33.7

38.3

Pindi matokeo yalipochambuliwa kwa kuzingatia kigezo cha umiliki wa shule, ilibainika kuwa ‘mazingiria mazuri ya kazi’ kilikuwa ndicho kigezo muhimu zaidi kilichowavutia walimu wa shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu, ilhali waalimu wa shule za kitaifa za serikali, shule za kata za serikali na shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kikristo kwa kiasi kikubwa walivutiwa na vigezo vinavyohusiana na ‘shauku na moyo wa kupenda kuwasaidia wengine’ (tazama Kielelezo 14).

Kielelezo 14: Vigezo vilivyowavutia walimu kuwa waalimu kwa kuzingatia umiliki wa shule

3.2.4 Moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu

Vipengele kumi na saba vilijumuishwa katika hojaji kuchunguza moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu. Matokeo yake yameelezwa kwa muhtasari katika Jedwali 4 na Jedwali 5. Kwa jumla, kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu kilikuwa cha chini. Mathalani, asilimia 40.6 tu ya waalimu ndiyo ‘waliokubaliana sana’ na ‘kukubaliana’ na kauli kwamba ‘Matamanio yangu ni kuendelea kuwa mwalimu’, huku asilimia 45.2 tu ya walimu ndio ‘wakikubaliana sana’ na ‘kukubaliana’ na kauli kwamba ‘Ninaiona kazi ya ualimu kuwa ya kuvutia sana na yenye kuridhisha mno’.

Zaidi ya hayo, asilimia 33.7 tu ndio walioarifu kuwa ‘Ninapenda maisha ya shuleni na niko radhi kufundisha kwa maisha yangu yote’, ilhali asilimia 35.3 tu ya waalimu ndio ‘waliokubaliana’ na kauli kuwa ‘Ikiwa nitapewa kuchagua kazi moja tu miongoni mwa nyinginezo, bado nitachagua kuwa mwalimu’. Kadhalika, asilimia 42.5 tu ndio ‘waliokubaliana sana’ na ‘kukubaliana’ na kauli kwamba ‘Ninaridhishwa sana na shule ninayofundisha’.

Jedwali 3: Moyo wa Kujitolea wa Waalimu kwa Kazi ya Ualimu

Maelezo

%

SA

A

N

D

SD

SA+A

SD+D

1. Matamanio yangu ni kuendelea kuwa mwalimu

12.9

27.7

22.8

17.5

17.2

40.6

34.7

2. Ninapenda kufundisha kuliko ilivyokuwa siku za nyuma

12.5

30.7

21.5

17.5

14.9

43.2

32.4

3. Ninapenda kufundisha somo nilipendalo kwa wanafunzi wangu

30.0

47.2

13.2

3.3

3.3

77.2

6.6

4. Niko radhi kusaidia kuendeleza shule yangu kadri niwezavyo

38.6

46.5

5.9

3.0

2.6

85.1

5.6

5. Hata wanafunzi wawe na tabia mbaya kiasi gani, bado nitajaribu kadri niwezavyo kuwafundisha

38.6

37.0

8.9

6.6

5.0

75.6

11.6

6. Ninaiona kazi ya ualimu kuwa ya kuvutia sana na yenye kuridhisha mno

16.5

29.7

18.5

17.2

14.2

46.2

31.4

7. Kazi ya ualimu ilikuwa/ni mojawapo ya machaguo yangu matatu ya kwanza ya kazi

22.1

36.3

15.5

11.9

10.6

58.4

22.5

8. Ualimu ni mgumu mno na hakuna faida ya maana unayoipata

23.8

24.8

17.5

18.8

12.2

48.6

31.0

9. Mitazamo na tabia za wanafunzi zimefifisha shauku yangu ya kufundisha

11.6

22.1

17.5

31.7

13.2

33.7

44.9

10. Kazi ya kufundisha ni ngumu mno kwangu na ninataka kuachana nayo

7.9

12.2

20.8

35.6

20.1

20.1

55.7

11. Ninapenda maisha ya shuleni na niko radhi kufundisha kwa maisha yangu yote

10.9

22.8

23.1

24.8

15.2

33.7

40.0

12. Sijakata tamaa; ninayo malengo ninayotaka kuyatimiza katika ualimu

14.9

17.8

18.8

27.7

17.5

32.7

45.2

13. Hata kukiwa na kazi nzuri zaidi, nitaendelea kufundisha

29.0

19.5

18.5

17.5

12.5

48.5

30.0

14. Kuthaminiwa kwangu na shule/mkuu wa shule kulinichochea kufanya kazi

10.9

30.0

23.8

16.8

13.9

40.9

30.7

15. Ikiwa nitapewa kuchagua kazi moja tu miongoni mwa nyinginezo, bado nitachagua kuwa mwalimu

10.2

25.1

24.4

18.2

18.2

35.3

36.4

16. Ninaridhishwa sana na shule ninayofundisha

15.5

37.0

21.8

12.5

10.2

52.5

22.7

17. Kwa jumla, ninapenda kuwafundisha wanafunzi wangu

32.0

46.5

11.2

4.0

3.6

78.5

7.6

Alama za wastani

19.9

30.2

17.9

16.7

12.0

50.0

28.8

Uchambuzi wa vigezo ulifanywa kuchunguza miundo ya ndani ya viwango vya moyo wa kujitolea walio nao waalimu ambapo vipengele hivi 17 vilifanyiwa uchambuzi wa sehemu kuu. Sehemu kuu tatu zilijitokeza zikiakisi hali tatu za viwango vya moyo wa kujitolea walio nao waalimu. Hali hizo tatu ni ‘moyo wa kujitolea walio nao waalimu na kuridhika kwao na kazi ya ualimu’, ‘moyo wa kujitolea walio nao waalimu katika kuwasaidia wanafunzi’ na ‘moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa shule na kuridhika kwao na shule’. Matokeo yake yameelezwa kwa muhtasari katika Kielelezo 15 na Kielelezo 16. Kielelezo 15 kinaonesha kiwango cha jumla cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu katika hali zote tatu na Kielelezo 16 kinaonyesha kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kuzingatia kigezo cha umiliki wa shule.

Kama Kielelezo 15 kinavyoonyesha, waalimu waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea wa hali ya juu katika kuwasaidia wanafunzi, ambapo asilimia 80.1 ya waalimu waliarifu kuwa na moyo wa kuwasaidia wanafunzi. Kiwango cha moyo wa kujitolea kwa kazi ya ualimu kilikuwa cha chini sana ambapo asilimia 36.6 tu ya waalimu ndio walioarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na kazi ya ualimu. Hali kadhalika, kiwango cha moyo wa kujitolea kwa ajili ya shule kilikuwa cha chini, ambapo asilimia 42.4 tu ya waalimu ndio walioarifu kuwa na moyo wa kujitolea kwa ajili ya shule walizokuwa wakifundisha.

Kielelezo 15: Idadi ya waalimu walioarifu kuwa na moyo wa kujitolea katika vipengele mbalimbali vya kazi ya ualimu

3.2.5 Kiwango cha moyo wa kujitolea wa waalimu kwa kigezo cha umiliki wa shule

Uchambuzi ulifanywa kuchunguza kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kuzingatia kigezo cha umiliki wa shule. Hii ilifanywa kwa kulinganisha kiwango cha moyo wa kujitolea na kuridhishwa na kazi ya ualimu miongoni mwa waalimu wa shule za serikali na za binafsi. Matokeo yake yameelezwa kwa muhtasari katika Kielelezo 16. Kwa jumla, waalimu wa shule binafsi za Kikristo walionyesha kuwa na moyo wa kujitolea wa hali ya juu na walioridhishwa na kazi ya ualimu kuliko waalimu wa shule nyinginezo. Mathalani, wakati asilimia 73 ya waalimu katika shule binafsi za Kikristo waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na kuridhishwa na kazi ya ualimu, pungufu ya asilimia 55 ya waalimu wa shule nyinginezo ndio walioarifu kuwa na moyo wa kujitolea na kuridhishwa na kazi ya ualimu.

Kiwango cha moyo wa kujitolea wa waalimu kwa shule walizofanyia kazi kilikuwa cha chini zaidi miongoni mwa waalimu wa shule binafsi zinazomilikiwa na watu binafsi na wale wa shule za kata za serikali, lakini kilikuwa cha juu kwelikweli miongoni mwa waalimu wa shule binafsi za Kikristo. Mathalani, wakati asilimia 71 ya waalimu wa shule binafsi za Kikristo waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na shule walizofundisha, asilimia 32 tu ya waalimu wa shule binafsi zinazomilikiwa na watu binafsi ndio walioarifu hivyo. Asilimia 36 tu ya waalimu wa shule za kata za serikali na asilimia 46 tu ya waalimu wa shule za kitaifa za serikali ndio walioarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na shule walizokuwa wakifundisha. Kwa kiasi fulani kulikuwepo pia na moyo wa kujitolea wa hali ya juu kwa shule miongoni mwa waalimu wa shule binafsi za Kiislamu, ambapo asilimia 56 ya waalimu wa shule hizi waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na shule walizofundisha.

Kielelezo 16: Moyo wa kujitolea wa waalimu na kuridhika kwao na shule walizofundisha[4]

Kwa jumla, na kwa wastani, asilimia 58.6 tu ya walimu walioshiriki katika utafiti ndio walioarifu kuwa walikuwa wameridhika na mazingira ya kazi katika shule walizokuwa wakifundisha. Pindi uchambuzi ulipofanywa kwa kuzingatia kigezo cha shule, kama Kielelezo 17 kinavyoonyesha, matokeo yalionyesha kuwa idadi kubwa zaidi kitakwimu (X2=[N=297, 12]=49.9, p<.0005) ya walimu wa shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kikristo (95%) na wale wa shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu (82%) waliarifu kuridhishwa na mazingira ya kazi ya shule zao kulinganisha na waalimu wa shule za kitaifa za serikali (59%), shule za kata za serikali (51%) na shule binafsi zinazomilikiwa na watu binafsi (51%).

Kielelezo 17: Idadi ya waalimu walioarifu kuridhishwa na mazingira ya kazi ya shule zao[5]

3.2.6 Moyo wa kujitolea na kuridhika na ualimu kwa kigezo cha jinsia

Uchambuzi ulifanywa pia kuchunguza kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kuzingatia jinsia yao. Cha kushangaza, ingawa tofauti haikuwa kubwa kitakwimu, idadi kubwa ya waalimu wa kiume waliarifu kuwa walikuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na masuala mbalimbali kuliko waalimu wenzao wa kike. Mathalani, kwa jumla, asilimia 55.4 ya waalimu wa kiume waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na kuridhika na kazi ya ualimu kulinganisha na asilimia 46 ya waalimu wa kike.

Pindi uchambuzi ulipofanywa kwa kuzingatia vipengele vitatu vya moyo wa kujitolea walio nao waalimu, matokeo yalionyesha mwelekeo unaofanana huku idadi kubwa ya waalimu wa kiume wakiarifu kuwa na moyo wa kujitolea kwa masuala mbalimbali katika kazi ya ualimu kuliko waalimu wa kike.

Mathalani, asilimia 38.5 ya waalimu wa kiume waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na wenye kuridhika na kazi ya ualimu, kulinganisha na asilimia 27 ya waalimu wa kike. Zaidi ya hayo, wakati asilimia 82 ya waalimu wa kiume waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea kuwasaidia wanafunzi, asilimia 76.5 ya waalimu wa kike ndio walioarifu hivyo. Kadhalika, asilimia 45.8 ya waalimu wa kiume waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na shule walizokuwa wakifundisha kulinganisha na asilimia 34.9 ya waalimu wa kike (tazama Kielelezo 18).

Kielelezo 18: Moyo wa kujitolea wa waalimu kwa kigezo cha jinsia

3.2.7 Moyo wa kujitolea na kuridhika na ualimu kwa kuzingatia uzoefu na masomo ya kufundisha

Uchambuzi ulifanywa kuchunguza kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kuzingatia uzoefu wa kufundisha na masomo ya kufundisha. Matokeo yake yameelezwa kwa muhtasari katika Jedwali 5.

Matokeo hayo yanaonesha kuwa, kwa wastani, waalimu wa masomo ya lugha walikuwa na moyo wa kujitolea zaidi na walioridhika zaidi na kazi ya ualimu kuliko walimu wa masomo ya sanaa na ya sayansi. Mathalani, asilimia 85.4 ya waalimu wa masomo ya lugha waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea katika kuwasaidia wanafunzi, kulinganisha na asilimia 78.1 ya waalimu wa masomo ya sanaa na asilimia 79.6 ya walimu wa sayansi. Kadhalika, asilimia 45.1 ya waalimu wa masomo ya lugha waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na shule walizokuwa wakifundisha, kulinganisha na asilimia 37.3 ya waalimu wa sayansi na asilimia 44.8 ya waalimu wa masomo ya sanaa. Lakini, idadi kubwa (39.9%) ya waalimu wa sayansi waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na kazi ya ualimu kuliko waalimu wa lugha (35.4%) na waalimu wa masomo ya sanaa (34.9%). Hata hivyo, uchambuzi uliofanywa kwa njia ya chi-square ulionyesha kutokuwepo kwa tofauti kubwa kitakwimu miongoni mwa makundi haya matatu ya waalimu.

Walimu kuwa na sifa nzuri kitaaluma hakukuashiria kwa namna mbalimbali kuwa na sifa ya moyo wa kujitolea katika kufundisha, kwani waalimu wenye sifa za kiwango cha chini waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea wa hali ya juu katika kufundisha kuliko waalimu wenye sifa za kiwango cha juu. Mathalani, idadi kubwa kitakwimu (64.3%) ya waalimu wa ngazi ya cheti waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na kazi ya ualimu kuliko wale wa ngazi ya stashahada (40.1%) na shahada (28.4%). Kadhalika, asilimia 93.3 ya waalimu wenye cheti cha ualimu waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea kuwasaidia wanafunzi, kulinganisha na asilimia 75.5 ya waalimu wenye stashahada na asilimia 79.6 ya waalimu wenye shahada. Hata hivyo, idadi kubwa ya waalimu wa ngazi ya shahada waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na shule walizokuwa wakifundisha kuliko waalimu wa ngazi ya stashahada (38.3%) na wa ngazi ya cheti (35.7%).

Jedwali 4: Moyo wa Kujitolea wa Waalimu kwa Masomo Wanayofundisha na Sifa za Kitaaluma

Masomo ya kufundisha

Uzoefu wa kufundisha

Sanaa

Lugha

Sayansi

p

Stashahada

Shahada

Cheti

p

1. Moyo wa kujitolea na kuridhika na kazi ya ualimu

34.9

35.4

39.9

0.70

40.1

28.4

64.3

0.03

2. Moyo wa kujitolea kusaidia wanafunzi

78.1

85.4

79.6

0.90

75.5

79.6

93.3

0.68

3. Moyo wa kujitolea kwa shule na kuridhika na shule

44.8

45.1

37.3

0.45

38.3

44.5

35.7

0.28

3.3 Ufanisi wa uongozi wa shule

Uongozi wa shule ni kigezo muhimu kinachoukilia kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu katika kufundisha. Katika utafiti huu, tuliwaomba waalimu kutathmini uongozi wa shule zao katika vipengele mbalimbali. Walipewa vifungu 12 vya maelezo na kuombwa kutathmini ni kwa kiasi gani walikubaliana na maelezo hayo kwa kuchagua jibu mojawapo kati ya majibu ya aina tano yaliyoanzia na ‘ninakubaliana sana’ hadi ‘sikubaliani kabisa’. Matokeo yake yameelezwa kwa muhtasari katika Jedwali 6 na Kielelezo 19.

Kama Kielelezo 19 kinavyoonyesha, ukiacha waalimu wa shule binafsi za Kikristo, maoni ya waalimu kuhusu kiwango cha ubora wa uongozi wa shule zao yalionyesha kuwa kilikuwa cha chini kabisa. Mathalani, kwa wastani, wakati asilimia 79.8 ya waalimu wa shule binafsi za Kikristo waliarifu kuwa uongozi wa shule zao ulikuwa ni wenye ufanisi katika masuala mbalimbali, asilimia 48 tu ya waalimu wa shule za kata za serikali, asilimia 37.9 tu ya waalimu wa shule binafsi za Kiislamu na asilimia 47 tu ya waalimu wa shule zinazomilikiwa na watu binafsi ndio waliokuwa na maoni sawa na hayo. Hivyo, ingawa tofauti haikuwa kubwa kitakwimu (X2= [N=266, 16]=16.82, p=.40), kulikuwa na tofauti za wazi kabisa katika maoni kuhusu ufanisi wa uongozi wa shule miongoni mwa waalimu wa shule za makundi hayo matano, ambapo idadi kubwa ya waalimu wa shule binafsi za Kikristo walikuwa na maoni yaliyounga mkono uongozi wa shule zao kuliko waalimu wa shule nyingine.

Kadhalika, pindi uchambuzi ulipofanywa kwa kuzingatia vipengele kadhaa, waalimu wa shule binafsi za Kikristo walipata alama za juu mno kuliko waalimu wa shule nyingine. Mathalani, wakati asilimia 76.2 ya waalimu wa shule binafsi za Kikristo ‘walikubaliana sana’ na pia ‘walikubaliana’ na mtazamo kwamba uongozi wa shule zao ‘hutengeneza mazingira mazuri ya kazi’, asilimia 49.1 tu ya waalimu wa shule za kitaifa za serikali, asilimia 37 tu wa shule za kata za serikali, asilimia 45.5 tu ya waalimu wa shule binafsi za Kiislamu na asilimia 35.9 tu ya waalimu wa shule za watu binafsi ndio waliokuwa na maoni sawa na hayo. Jambo la kuvutia, hata hivyo, ni kwamba idadi kubwa ya waalimu wa shule binafsi za Kiislamu walikuwa na maoni chanya kuhusu vipengele viwili vya kupima ufanisi wa uongozi wa shule, navyo ni ‘(uongozi wa shule) husisitiza nidhamu ya kiwango cha juu’ na ‘(uongozi wa shule) ni mfano wa kuigwa’. Mathalani, asilimia 72.7 ya waalimu wa shule hizi ‘walikubaliana sana’ au ‘walikubaliana’ na kauli kwamba uongozi wa shule zao ‘ni mfano wa kuigwa’.

Jedwali 5: Asilimia ya Waalimu Waliotathmini Ufanisi wa Uongozi wa Shule Zao

% ‘Ninakubaliana Sana’ na ‘Ninakubaliana’

Maelezo

Serikali-Kitaifa

Serikali-Kata

Binafsi-Kikristo

Binafsi-Kiislamu

Binafsi-Watu

1. Hutengeneza mazingira mazuri ya kazi

49.1

37.0

76.2

45.5

35.9

2. Huhakikisha kuna umoja/ushirikiano baina ya uongozi/ waalimu/ watumishi/ jamii

57.7

54.3

81.0

18.2

48.7

3. Una mipango kabambe, utaratibu mzuri

55.2

49.1

85.7

0

46.2

4. Huhamasisha kushiriki katika kuendesha masuala ya shule

52.7

53.4

81.0

27.3

48.8

5. Huchochea ushirikiano

60.3

48.3

85.7

45.5

59.0

6. Huruhusu kupata taarifa kirahisi

55.2

49.1

76.2

27.3

50.0

7. Huonyesha kuwa na sifa za juu za uongozi

50.9

44.8

66.6

27.3

51.3

8. Hufanya tathmini ya mara kwa mara na ya haki kwa watumishi

54.3

45.7

76.2

36.4

38.5

9. Huhakikisha kuna vifaa bora vya kufundishia na kujifunzia

55.2

48.3

76.2

45.5

41.0

10. Husisitiza nidhamu ya kiwango cha juu

62.1

56.9

90.5

72.7

56.4

11. Ni mfano wa kuigwa

51.8

43.1

80.9

72.8

43.6

12. Huonyesha sifa za kuigwa za mwalimu mzuri

60.4

46.5

81.0

36.4

53.8

Wastani

55.4

48.0

79.8

37.9

47.8

Kielelezo 19: Idadi ya waalimu ‘waliokubaliana sana’ na ‘waliokubaliana’ na kauli kuwa uongozi wa shule yao una ufanisi

3.4 Muhtasari: Uhusiano uliopo baina ya ufaulu wa shule kitaaluma na sifa za walimu kitaaluma, moyo wao wa kujitolea kwa kazi ya ualimu na maoni yao kuhusu ufanisi wa uongozi wa shule

Kwa matokeo ya hapo juu, ni dhahiri kuwa vipengele vitatu vinaonyesha kuwa ni muhimu zaidi katika kuukilia ufaulu wa shule kitaaluma. Vipengele hivyo ni sifa za waalimu kitaaluma, moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu na mtazamo wao chanya kuhusu ufanisi wa uongozi wa shule. Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha dhahiri kuwa waalimu wenye sifa nzuri kitaaluma wanao uwezo wa kuwafanya wanafunzi kufaulu vizuri, lakini hii inawezekana ikiwa tu vigezo vingine vitatiliwa maanani, navyo ni moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi yao na vilevile kuridhishwa kwao na uongozi wa shule. Hii ina maana kuwa kuboresha sifa za waalimu kitaaluma hakuna budi kwenda bega kwa bega na kuboresha mazingira ya kazi ya waalimu na ufanisi wa uongozi wa shule ili waalimu waweze kuifurahia kazi yao na hivyo kuboresha moyo wao wa kujitolea kazini.

Hata hivyo, pindi uchambuzi ulipofanywa kwa njia ya chi-square, moyo wa kujitolea walio nao waalimu na maoni yao kuhusu ufanisi wa uongozi wa shule ndivyo vigezo pekee vilivyoonyesha kuleta matokeo muhimu kitakwimu.

3.5 Maoni ya waalimu kuhusu kazi ya ualimu: Matokeo ya Majadiliano ya Vikundi

3.5.1 Utangulizi

Ili kutimiliza utafiti uliofanywa kwa njia ya hojaji, waalimu walipewa fursa ya kubadilishana uzoefu wao kuhusu kazi ya ualimu na mazingira yao ya kazi kwa jumla kupitia majadiliano ya vikundi lengwa. Majadiliano yalifanywa kwa kikundi walau kimoja katika kila shule iliyoshiriki, na kila kikundi kilikuwa na washiriki kuanzia watano (5) hadi tisa (9). Majadiliano haya ya vikundi lengwa yalirekodiwa kwenye vinasa sauti na kunakiliwa neno kwa neno katika maandishi. Kisha majadiliano yaliyonakiliwa yalifanyiwa uchambuzi wa kimaudhui, ambapo maudhui makuu yalibainishwa na kufafanuliwa kwa kutumia nukuu za washiriki.

Maudhui makuu manne yalibainishwa, nayo ni: (i) kwa nini waalimu walichagua kazi ya ualimu; (ii) mitazamo ya waalimu kuhusu kazi ya ualimu; na (iii) maoni ya waalimu kuhusu sababu za wanafunzi kufanya vibaya kitaaluma na nini kifanyike kuboresha kiwango cha elimu na kiwango cha ufundishaji.

3.5.2 Kwa nini waalimu walichagua kazi ya ualimu

Uchambuzi wa majadiliano ya vikundi lengwa ulibainisha sababu kuu tano zilizowavutia waalimu kuchagua kazi ya ualimu. Sababu ya kwanza na iliyo muhimu zaidi ni urahisi wa kupata ajira waliouona waalimu baada ya kuhitimu mafunzo. Waalimu wengi walieleza kwamba walichagua kazi ya ualimu kwa sababu waliamini kuwa ingekuwa rahisi kwao kupata ajira baada ya kumaliza masomo yao kulinganisha na kazi nyingine. Walimu walieleza pia kwamba kazi ya ualimu iliwapa uhakika mkubwa zaidi wa kusaidia familia zao kwani kuna uhakika wa kupata ajira mara tu mtu anapohitimu mafunzo yake. Nukuu za maoni ya baadhi ya washiriki zilizopo hapa chini zinathibitisha hili:

Nadhani sababu kubwa iliyonifanya kuchagua kazi hii (ualimu) ilikuwa ni ukweli kwamba nilifikiri itakuwa rahisi kupata ajira baada ya masomo yangu. Lakini kama ingewezekana kupata ajira katika fani nyingine, kamwe nisingeweza kuchagua kazi ya ualimu (Mwalimu, Shule A1, Mkoa wa Pwani).

Nilichagua kuwa mwalimu kwa sababu nilijua ilikuwa rahisi kupata kazi katika sekta ya elimu. Nina ndugu wengi ambao walisomea kozi nyingine na niliwaona walivyohangaika kupata ajira; sikutaka kuhangaika kama wao, kwa hiyo nikaamua kuwa mwalimu. Lakini ualimu siyo kazi ninayopanga kuifanya kwa muda mrefu; mwishowe nitaachana na kazi hii (Mwalimu, Shule Z, Mkoa wa Pwani).

Kwa kweli, nilikuwa mwalimu kwa bahati mbaya tu! Ni kwa sababu ilikuwa rahisi zaidi kwangu kupata kazi. Lakini, kwa kweli, baada ya kujiunga na kazi hii, hakuna kitu ambacho kweli kinanihamasisha kuendelea kuwa mwalimu. Ni suala la wakati tu; bila shaka nitaachana na kazi hii (Mwalimu, Shule H, Mkoa wa Dodoma).

Mtu asikudanganye. Tupo hapa kwa sababu tulitaka ajira na ualimu ndiyo njia rahisi zaidi ya kupata kazi (Mwalimu, Shule D, Mkoa wa Singida).

Sababu ya pili iliyotajwa mara kwa mara kama kigezo kilichowafanya waalimu kuchagua kazi hii ilikuwa ni kutokuwa na sifa za kujiunga na kazi nyingine. Waalimu walieleza kuwa baadhi yao walichagua kazi ya ualimu baada ya kushindwa kupata sifa zinazohitajika kujiunga na kazi nyingine, kama vile katika sekta ya fedha, uchumi, tiba, uhandisi, na kadhalika. Hivyo, waliona kuwa kazi ya ualimu ingekuwa njia ya kupatia kazi nyingine wazipendazo. Kwa sababu hiyo, ualimu ulichukuliwa zaidi kuwa ni kazi ‘ya mpito tu’ wakati mtu akisubiria kazi nyingine nzuri ijitokeze. Ni dhahiri kuwa hali hii huwafanya waalimu kutojihusisha sana na kazi ya ualimu na kutokuwa na moyo wa kujitolea kwa kazi hii. Nukuu chache za maoni zilizopo hapa chini zinathibitisha hili:

Watu huchagua kazi hii (ualimu) kama chaguo la mwisho – wameshindwa kupata kitu kingine chochote cha maana maishani mwao na, kwa hiyo, kazi ya ualimu ndilo chaguo pekee lililobaki. Mimi ni mfano halisi: niko hapa kwa sababu matokeo yangu ya kidato cha sita yalikuwa ovyo. Nilitaka kusomea Uchumi, lakini matokeo yangu hayakuniruhusu. Vinginevyo, kamwe nisingekuwa mwalimu (Mwalimu, Shule Z1, Mkoa wa Pwani).

...Halafu, hii ndiyo kazi pekee ambayo mtu yeyote anaweza kujiunga nayo. Ukifeli, huku ndiko unakoishia. Kwa hiyo niko hapa kwa sababu, kwa kweli, nilishindwa kupata matokeo mazuri ya kujiunga na kazi nyingine. Ningeenda wapi kwingine na matokeo yangu mabaya kwa kila somo nililofanya? Kwa mfano, nilikuwa na ‘credit’ mbili tu, zote zilikuwa ‘E’; ningeenda wapi kwingine kama siyo Diploma ya Ualimu? (Mwalimu, Shule D, Mkoa wa Singida)

Ualimu haukuwa chaguo langu la kwanza. Chaguo langu la kwanza lilikuwa utalii, na nilichagua ualimu kama chaguo la tatu. Nililazimishwa kuwa mwalimu; walinipa chaguo la tatu. Tangu hapo nimekuwa sina furaha (Mwalimu, Shule A, Mkoa wa Singida).

Kwa upande wangu, nilijiunga na kazi ya ualimu kwa sababu nilipata Daraja la Tatu na sikupata alama nzuri za kuniwezesha kujiunga na kidato cha tano, kwa hiyo ilibidi niende Diploma ya Ualimu. Kwa hiyo ualimu haukuwa chaguo langu hata kidogo, lakini mazingira yamenilazimisha kujiunga nao kwa sababu ya matokeo yangu mabaya. Lakini kama kitu kingine kizuri kikijitokeza, nitaachana mara moja na kazi hii bila kujiuliza maswali (Mwalimu, Shule J, Mkoa wa Dodoma).

Ingawa waalimu wengi walioshiriki katika majadiliano haya ya vikundi walitaja sifa duni kitaaluma na urahisi wa kupata ajira kuwa ndizo sababu kuu zilizowavutia kuchagua kazi ya ualimu, waalimu wengine wachache walitaja sababu nyingine kama vile ‘kupenda kwa mtu na kuvutiwa na watu wengine mashuhuri’. Baadhi ya waalimu walieleza kwamba walichagua kazi ya ualimu kwa sababu waliipenda kazi hii na waliamini ilikuwa ndiyo njia bora zaidi ya kuitumikia jamii. Aidha, waliiona kazi ya ualimu kuwa ni kazi ya uadilifu iliyohitaji watu waadilifu.

Waalimu wengine walieleza kuwa walichagua kazi ya ualimu kwa sababu ya kuvutiwa na wazazi na/au ndugu wengine wa karibu. Walidai kwamba walichagua kazi ya ualimu kwa sababu tu wazazi wao au watu wengine wa karibu waliokuwa wa muhimu kwao walikuwa waalimu. Zaidi ya hayo, waalimu wengine walisema kuwa walichagua kazi ya ualimu kwa sababu walishauriwa kufanya hivyo na watu wengine wa muhimu kwao. Hapa chini kuna baadhi ya nukuu zinazothibitisha maoni hayo:

Ninaipenda Historia, na niliona kwamba kuwa mwalimu wa Historia ingekuwa ni njia bora zaidi ya kupanua maarifa yangu katika eneo hili (Mwalimu, Shule J, Mkoa wa Dodoma).

Ninapenda tu kufundisha wengine; kwa hiyo kujiunga na kazi ya ualimu lilikuwa ni chaguo langu kwa asilimia mia moja kwa sababu ninapenda ualimu (Mwalimu, Shule Z, Mkoa wa Pwani).

Kwangu mimi, ni kwa sababu nilivutiwa na mazingira niliyokuwemo. Kijiji ninachotoka ualimu ndiyo kazi pekee ambayo watu wanaijua, kwa hiyo kila mtu ni kama anapenda ualimu, na mimi ni zao lake (Mwalimu, Shule M, Mkoa wa Kigoma).

‘Nilirithi’ kutoka kwa wazazi wangu. Wazazi wangu wote, baba na mama, ni waalimu na nilikua nikiwa ninaupenda ualimu, na kwa kweli nina furaha kuwa mwalimu (Mwalimu, Shule T, Mkoa wa Mtwara).

Siipendi kazi ya ualimu. Nilitaka kusomea utawala, lakini wazazi wangu walinishauri kusomea elimu maalumu, nikakubali na nilikuwa ninategemea kwamba ningefundisha watoto wenye mahitaji maalumu. Lakini nipo hapa, nikifanya mambo ambayo kamwe sikutaka kuyafanya. Badala ya kunipeleka kwenye shule maalumu ambako ningeweza kufundisha wanafunzi wenye ulemavu, walinileta hapa, na kunilazimisha kufundisha somo ambalo kamwe sikulitaka (Mwalimu, Shule A, Mkoa wa Singida).

3.5.3 Mitazamo ya waalimu kuhusu kazi ya ualimu

Uchambuzi wa majadiliano ya vikundi lengwa vya waalimu ulionyesha masuala kadhaa yanayoweza kuchukuliwa kuwa ndiyo mitazamo waliyo nayo kuhusu kazi ya ualimu. Mitazamo hiyo inaweza kuwekwa katika makundi makuu mawili, nayo ni mitazamo chanya na mitazamo hasi. Hapa tutaonyesha baadhi ya mitazamo iliyo muhimu.

Mitazamo chanya (sababu zinazotia hamasa)

Mitazamo kadhaa chanya au sababu zinazotia hamasa kuhusu kazi ya ualimu zilibainishwa katika majadiliano haya. Kwanza, waalimu walieleza kwamba walifurahia ukweli kwamba kazi ya ualimu iliwapa fursa ya kuendelea kujifunza. Walidai kuwa ni ualimu pekee unaomwezesha mtu kujifunza na kuongeza upeo wa maarifa yake kila mara. Pili, waalimu walibainisha pia ukweli kwamba ilikuwa rahisi zaidi kwa waalimu kujiendeleza zaidi kimasomo kulinganisha na kazi nyingine. Hivyo basi, hali hii iliwapa uwezekano wa kujiendeleza katika kazi zao na vilevile urahisi wa kubadili kazi. Tatu, waalimu waliona kuwa walisikia faraja pindi kazi yao ilipothaminiwa, hususan na wanafunzi waliowafundisha. Waliona kuwa wanafunzi wengi walithamini kazi yao. Nne, uwezekano wa kukutana na watu mbalimbali na kujipatia marafiki wapya ulichukuliwa kuwa ni jambo chanya. Hapa chini kuna baadhi ya nukuu zinazothibitisha mitazamo hiyo:

Ualimu umekuwa mzuri kwangu kwa sababu ninapata marafiki na kukutana na watu wapya kila siku. Vilevile unatupatia fursa ya kujua maisha halisi ya Tanzania: nimeona jinsi nchi hii ilivyo maskini na tajiri kupitia kwa watoto ninaowafundisha. Huu ni uzoefu mzuri kwangu mimi (Mwalimu, Shule Z1, Mkoa wa Pwani).

Kitu kizuri kuhusu ualimu ni kwamba inabidi usome kila siku. Aina ya watoto tunaowafundisha siku hizi ‘inatulazimisha’ kusoma. Kwa kuwa wanajua mambo mengi, usipopiga msasa akili yako, utakuwa kichekesho darasani. Kwa hiyo katika ualimu inabidi usome kila siku na hii ni nzuri kwangu (Mwalimu, Shule U, Mkoa wa Mtwara).

Wakati pekee ninaoufurahia katika kazi hii ni pale ninapoona wanafunzi wangu wakifanya vizuri katika somo langu, nitaenda kuwaambia wenzangu na pale unapoonana na mkuu wa shule na kuona anatabasamu; na hii inanifanya nijisikie vizuri (Mwalimu, Shule H, Mkoa wa Dodoma).

Inaleta faraja; ni vizuri kujua kuwa na mimi pia ninachangia kuboresha maisha ya mtu na kwamba mimi pia ninajenga taifa (Mwalimu, Shule C, Mkoa wa Singida).

Mitazamo hasi (sababu zinazovunja moyo)

Walimu walibainisha mitazamo mingi hasi katika kazi ya ualimu, ambayo pia inaweza kuelezwa kuwa ni sababu zinazoondoa hamasa au sababu ‘zinazovunja moyo’. Mitazamo hii kwa kiasi kikubwa ilihusu maeneo makuu mawili, nayo ni mazingira duni ya kazi na mtazamo hasi kuhusu kazi ya ualimu (walio nao wanajamii, wanafunzi na hata serikali). Hapa chini tumeonyesha na kufafanua baadhi ya hisia muhimu za moyoni walizo nazo waalimu kuhusu maeneo haya.

Walimu wengi walilalamika kwamba wanafunzi wao hawawapi heshima wanayostahili walimu wao na walikuwa na mitazamo hasi sana kuhusu kazi ya ualimu. Hii ilijitokeza zaidi katika baadhi ya shule binafsi ambazo huchukua wanafunzi wanaotoka katika familia zenye uwezo. Kwa mujibu wa waalimu, wanafunzi wa shule hizi waliamini kuwa waalimu wao wanafanya kazi ya ualimu kwa sababu ni maskini. Hapa chini kuna maoni ya baadhi ya waalimu kuhusu suala hili:

...wanafunzi wananiona kama ‘nimechemsha’, mtu ambaye nimepotea. Wanaamini mwalimu ni mtu maskini, hana mwelekeo maishani. Kuna wakati wanafunzi wananiuliza, “Mwalimu, una akili sana, lakini sasa kwa nini uliamua kuwa mwalimu?” Maswali ya aina hii yanakera. Ina maana wanaamini mwalimu ni mtu aliyefeli, asiye na akili. Ninapowaambia, “Nilipenda tu kuwa mwalimu”, wananiambia, “Huoni kwamba ‘unachelewa katika maisha’?” Haya ndiyo maisha tunayoishi katika shule hii (Mwalimu, Shule Z, Mkoa wa Pwani).

Ahaa, haa! Ngoja nikuambie kitu ... kuna mwanafunzi mmoja darasani mwangu ambaye ana akili kwelikweli. Siku moja, ehee, nilimwambia, “Utakuwa mwalimu mzuri sana.” Kauli hiyo ilimfanya alie sana. Nikashangaa kwa nini analia. Baadaye akaniambia kamwe hataki kuwa mwalimu, na kwamba nilikuwa ninamtakia mabaya kumwambia atakuwa mwalimu mzuri. Nilijisikia vibaya sana (Mwalimu, Shule Z, Mkoa wa Pwani).

Ama kuhusu mitazamo ya jamii na serikali kuhusu waalimu, waalimu walisema:

Hii ni kazi ngumu sana. Hakuna anayejali – si jamii ambako unafundisha, si serikali. Jamii inatuona tumepotea, hatuna la maana na tutaishia kushindwa. Jamii inafanya maisha yetu hapa kuwa ya ovyo sana kwa sababu hawathamini kile tunachokifanya. Halafu, mzazi wetu, serikali, ndiyo mbaya zaidi. Wanawatupa tu mashuleni, wanaacha hivyo tu. Hakuna anayejali – hakuna nyumba, hakuna usafiri. Unahangaika hata kupata mshahara wako; wala sizungumzii mishahara kuwa midogo sana. Kuchagua kuwa mwalimu ni kuchagua kuhangaika maisha yako yote (Mwalimu, Shule C, Mkoa wa Singida).

Pengine sababu zinazovunja moyo zilizobainishwa zaidi ni zile zilizohusiana na mazingira duni ya kazi kama yanavyodhihirishwa na kuwepo kwa mishahara midogo na ukosefu wa zana za kufundishia na kujifunzia. Waalimu wengi walizungumza kwa ukali kuhusu mishahara midogo waliyolipwa, na vilevile ukweli kwamba shule nyingi hazikuwa na zana muhimu za kufundishia. Waalimu pia ‘walilia’ kwa ukali kuhusu ukosefu wa programu za mafunzo kazini. Huku wakikosoa zaidi, walisema kuwa pindi fursa za aina hiyo zinapotokea, wakuu wa shule zao ndio wanaohudhuria kwani zina marupurupu.

3.5.4 Mitazamo ya waalimu kuhusu wanafunzi kufanya vibaya kitaaluma na nini kifanyike kuboresha kiwango cha elimu

Katika sehemu ya mwisho ya majadiliano ya vikundi lengwa, washiriki waliombwa kubainisha mambo waliyodhani kuwa yalisababisha wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani ya taifa, hususan wakitilia maanani Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ya mwaka jana. Waliombwa pia kupendekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa kurekebisha hali hiyo na kuboresha kiwango cha elimu nchini kwa jumla.

Mambo makuu mawili yalibainishwa kuwa ndiyo husababisha wanafunzi kufanya vibaya. Kwanza, waalimu walio wengi walitaja mazingira duni ya kazi kuwa ndiyo sababu kuu ya kufanya vibaya. Waalimu walieleza bayana kwamba kwa mazingira duni ya kazi yaliyopo, waalimu hawakuwa wakifundisha kwa uwezo wao wote na kwamba mazingira ya shule yalikuwa yakiwavunja moyo katika kutimiza wajibu wao kwa ukamilifu na kwa ufanisi. Masuala makuu matatu yalitajwa bayana kuwa yalisababisha kuwepo kwa mazingira duni ya kazi. Masuala hayo ni uduni wa mishahara na marupurupu mengine ya waalimu, ukosefu wa zana za kufundishia na kujifunzia na uongozi na usimamizi mbaya wa shule.

Pengine mishahara duni ndiyo sababu iliyokuwa ikiwavunja moyo zaidi waalimu walio wengi. Walidai, kwa mfano, kuwa mwalimu mwenye shahada alikuwa akipata mshahara ulio pungufu ya shilingi 500,000/- anapoajiriwa kwa mara ya kwanza, nao wakajiuliza ni waajiriwa wengine wangapi wa serikali wenye kiwango cha elimu kilicho sawa na hicho ambao humudu kuendesha maisha yao kwa mwezi kwa kiwango hiki cha mshahara? Walisema vilevile kwamba, licha ya mishahara midogo waliyokuwa wakiipata, kuna makato mengi yanayozidi kupunguza kipato halisi wanachopokea.

Vilevile kulikuwa na suala la kupandishwa madaraja kazini. Waalimu wengi walilalamika kuwa upandishaji wa madaraja hufanywa na mamlaka kama fadhila badala ya haki stahili ya mwalimu kulingana na sifa njema alizo nazo. Waalimu walilalamikia zaidi urasimu mwingi uliopo katika kupandishwa daraja, na vigezo vinavyotumiwa kumpandisha mwalimu daraja havikuwa wazi, jambo linalofanya mchakato mzima kuwa na walakini. Mathalani, waalimu walilalamika kuwa ili waweze kufikiriwa kupandishwa daraja, inawapasa ‘kuwa wema na kuwa karibu’ na maofisa wa Idara ya Huduma kwa Walimu (TSD), chombo kinachoshughulikia masuala ya kitaaluma ya waalimu, ikiwa ni pamoja na upandishaji wa madaraja.

Pia, waalimu walilalamikia kuwepo kwa upungufu wa nyumba, hali iliyowalazimu kuishi maisha duni sana kwani hawakuweza kumudu gharama za makazi mazuri mijini kwa sababu ya mishahara duni waliyoipata. Tatizo la makazi duni lilikuwa kubwa zaidi kwa shule za vijijini, hususan shule za kata za serikali. Shule nyingi za kata za serikali zilizotafitiwa hazikuwa na huduma ya umeme na hii ilifanya maisha ya waalimu kuwa duni zaidi. Hapa chini kuna nukuu za maoni ya baadhi ya waalimu zinazothibitisha hali hiyo:

...Kama unavyoona shule yetu iko kilometa 20 kutoka mjini. Hakuna umeme hapa, hakuna nyumba za waalimu. Tunatakiwa kupanga nyumba kwa wenyeji, lakini nyumba zenyewe umeziona? Hivi, serikali hii inatufikiriaje? Hivi hawajui kuwa na sisi ni binadamu, tumesoma na tunataka maisha mazuri? Na mimi ninapenda kuona Manchester wakicheza, lakini ona: niko hapa, hakuna umeme, hakuna usafiri kwenda mjini, na unataka nifundishe kwa furaha? (Mwalimu, Shule C, Mkoa wa Singida.)

Ni bahati mbaya tu kuwa mwalimu katika nchi hii. Unapokea mshahara mdogo sana, na mshahara huohuo unakatwa vibaya mno, makato mengi mno, ehee. Kwa mfano, kwa nini mchango wangu wa bima ya afya uongezeke pale mshahara wangu unapoongezeka? Kwa nini wasiendelee na kiwango kilekile, ukizingatia kwamba hata huwa siumwi kila siku? Kwa nini inakuwa hivi kwa waalimu? (Mwalimu, Shule U, Mkoa wa Mtwara.)

Ufundishaji duni na vifaa/zana duni za kufundishia ilikuwa ni sababu nyingine iliyotajwa mara kwa mara ya wanafunzi kufanya vibaya kitaaluma. Waalimu walilalamika kuwa shule zao kwa jumla hazikuwa katika hali nzuri ya kuwezesha ufundishaji na ujifunzaji kufanyika. Mitazamo ya waalimu katika eneo hili kwa kiasi kikubwa ilithibitisha matokeo ya utafiti uliofanywa kwa njia ya hojaji na miongozo ya taarifa za shule. Mathalani, shule nyingi hazina maabara na maktaba zinazofaa. Kadhalika, masomo mengi hayakuwa na vitabu vya kutosha vya kiada na ziada. Kwa sababu hiyo, ufundishaji uliachwa ufanywe kwa kutegemea juhudi za mwalimu mwenyewe, na hili halingewezekana ukitilia maanani kiwango cha chini cha hamasa na moyo wa kujitolea kilichopo katika kazi ya ualimu. Kwa mfano, waalimu walikuwa na maoni kama:

Shule zimekuwa mahali pa vijana kukulia, hakuna ujifunzaji unaofanyika. Hakuna maktaba hapa, hakuna maabara, hakuna vitabu. Waalimu wamechoka na wana huzuni wakati wote. Sasa utaiita hii shule, hee? (Mwalimu, Shule A, Mkoa wa Singida.)

Hata hivyo, licha ya kukosolewa sana kwa hali duni ya mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, kulikuwa vilevile na maoni chanya katika shule chache, hususan shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kikristo. Katika shule hizi, hali ya zana za kufundishia na kujifunzia, kama ilivyoonyeshwa katika matokeo ya utafiti kwa njia ya hojaji, ilikuwa nzuri mno na yenye kutia moyo kuliko katika shule nyinginezo. Kwa sababu hiyo, waalimu wa shule hizi waliamini kuwa shule zao zilikuwa zikifanya vizuri zaidi katika mitihani kwa sababu zilikuwa na mazingira yanayofaa na yenye kurahisisha mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji. Kwa mfano, mwalimu mmoja, ambaye aliungwa na mkono kwa kauli moja na wengine katika kipindi cha majadiliano ya vikundi lengwa, aliyetoka katika shule moja ya binafsi ya Kikristo mkoani Singida, alikuwa na maoni haya:

Kwa jumla matokeo katika shule yetu ni mazuri. Hii ni kwa sababu shule ina zana bora za kufundishia na kujifunzia, zikiwemo maabara. Vilevile tuna maktaba nzuri sana. Vilevile waalimu wanahudhuria mara kwa mara programu mbalimbali za mafunzo zinazolenga kuboresha ufundishaji wao na kubadilishana mawazo na ujuzi, ambazo huandaliwa na Tume ya Huduma za Jamii ya Kikristo.

Jambo jingine lililotajwa kusababisha wanafunzi kufanya vibaya kitaaluma lilikuwa ni uongozi na usimamizi mbaya wa shule. Walimu walio wengi katika shule nyingi zilizotafitiwa walikosoa uongozi wa shule zao, wakidai kuwa haukuwa makini na mahitaji ya waalimu. Waalimu pia walitoa maoni kwamba kulikuwa na mawasiliano duni kati ya waalimu na uongozi wa shule zao. Wakikosoa zaidi, waalimu walitoa maoni kwamba hapakuwa na utaratibu wa kutathmini kazi za waalimu hata pale walipofanya kazi kwa uwezo wao wote katika mazingira magumu sana, badala yake uongozi wa shule ulikuwa mwepesi kuwalaumu waalimu pindi wanafunzi walipofanya vibaya katika mitihani. Hapa chini kuna nukuu za maoni ya baadhi ya waalimu kuhusu uongozi wa shule zao:

Uongozi wetu ni tatizo kubwa. Kwa mkuu wetu wa shule, maendeleo ya taaluma ni suala lisilo muhimu sana. Hajali kama kuna zana za kufundishia au la. Halafu, kuna mawasiliano duni sana kati yetu (waalimu) na yeye: ni vigumu sana kumwona, hakuna mikutano. Anajifanyia kila kitu yeye mwenyewe (Mwalimu, Shule A, Mkoa wa Singida).

Uongozi wetu wa shule hauko makini katika kushughulikia matatizo ya waalimu. Hakuna usimamizi wa shughuli za ufundishaji, hakuna semina kwa waalimu, hakuna anayejali. Mwalimu anaweza kufundisha kwa mwaka mzima bila kuwa na andalio la somo, na hakuna atakayekuuliza. Shule haina mwenyewe! (Mwalimu, Shule A, Mkoa wa Singida.)

Msingi duni wa wanafunzi kitaaluma na kitabia ni jambo jingine lililotajwa kusababisha wanafunzi kufanya vibaya kitaaluma. Hali hii ilihusishwa zaidi na ukosefu wa maarifa ya msingi yanayohitajika ili kumudu elimu ya sekondari. Waalimu walitoa maoni kwamba wanafunzi wengi wanaojiunga na elimu ya sekondari, hususan shule za kata za serikali, wana msingi duni sana wa kitaaluma kiasi kwamba hawawezi kumudu matakwa ya elimu ya sekondari. Kwa mfano, waalimu walitoa maoni kwamba kiwango cha ujuzi wa kusoma na kuandika cha wanafunzi wengi kilikuwa cha chini sana huku baadhi ya wanafunzi wakiwa hawajui kusoma na kuandika. Zaidi ya hayo, baadhi ya wanafunzi walikuwa na ufahamu mdogo sana wa lugha ya Kiswahili. Ni dhahiri kwamba hili ni tatizo kubwa kwa sababu ikiwa wanafunzi hawawezi kuwasiliana kwa ufasaha kwa Kiswahili pindi wanapojiunga na elimu ya sekondari, watatarajiwa vipi waweze kumudu masomo yao ya sekondari yanayofundishwa kwa lugha ya Kiingereza? Hapa chini kuna nukuu za maoni ya baadhi ya waalimu zinazothibitisha hali hii:

...kuna wanafunzi wengi wasiojua kusoma na kuandika katika shule yetu. Ninafundisha kidato cha kwanza, na ninafahamu karibu wanafunzi kumi ambao hawajui kusoma wala kuandika. Sasa, unategemea mimi nitawasaidiaje? (Mwalimu, Shule U, Mkoa wa Mtwara.)

Hii ni shule ya kata (ya serikali). Tunapokea wanafunzi duni sana, na kwa kweli tunapokea makombo: wale ambao hawakuweza kuchaguliwa na shule za kitaifa za serikali. Wengi wa wanafunzi tunaowapokea hawawezi kuandika vizuri, ujuzi wao wa Kiingereza ni mdogo sana na wanahitaji muda mwingi ili waweze kumudu elimu ya sekondari (Mwalimu, Shule D, Mkoa wa Singida).

4. Muhtasari, Hitimisho na Mapendekezo

4.1 Muhtasari

Kwa kutumia mikabala yote miwili, mkabala wa kiidadi na mkabala wa kiubora, utafiti huu umechunguza jinsi sifa za waalimu kitaaluma, hamasa na moyo wa kujitolea walio nao katika kufundisha vinavyoathiri ufaulu wa wanafunzi kitaaluma katika elimu ya sekondari. Utafiti huu ulifanywa katika mikoa sita (6) katika shule 36, ukishirikisha waalimu zaidi ya 300 kutoka shule za sekondari za serikali na za binafsi. Waalimu walishiriki katika utafiti huu kwa kujaza hojaji na kupitia majadiliano ya vikundi lengwa.

Matokeo ya utafiti huu yameonyesha kuwepo kwa masuala kadhaa yanayohusiana na sifa za waalimu kitaaluma, hamasa na moyo wa kujitolea kufundisha walio nao waalimu na jinsi masuala hayo yanavyoathiri ufaulu wa wanafunzi kitaaluma. Masuala hayo yanajumuisha haya yafuatayo:

i) Sifa za waalimu kitaaluma, hamasa na moyo wa kujitolea walio nao katika kufundisha ni vigezo muhimu mno vinavyoukilia ufaulu wa wanafunzi kitaaluma. Mwalimu kuwa na sifa nzuri za kitaaluma pekee bila moyo wa kujitolea hakusababishi kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi kitaaluma kuimarika.

ii) Shule zenye waalimu wenye moyo wa kujitolea wa hali ya juu bila kujali iwapo walikuwa na sifa za juu kitaaluma (shahada au zaidi) au la zilifanya vizuri katika mitihani ya taifa. Kwa upande mwingine, shule zenye waalimu wenye sifa za juu kitaaluma lakini wenye kiwango kidogo cha moyo wa kujitolea katika kazi ya ualimu si lazima kwamba zilifanya vizuri katika mitihani ya taifa kuliko zile zenye waalimu wenye sifa za wastani kitaaluma (stashahada au chini). Hivyo, kwa mfano, shule za serikali zenye idadi kubwa zaidi ya waalimu wenye sifa za juu kitaaluma hazikufanya vizuri kama shule binafsi za Kikristo zenye idadi ya chini kiasi ya waalimu wenye sifa za juu kitaaluma.

iii) Mazingira mazuri ya kazi ndicho kigezo muhimu zaidi kinachoukilia kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu katika kufundisha, na matokeo yake kigezo hiki huwa na nguvu sana katika kuleta matokeo mazuri ya wanafunzi kitaaluma. Matokeo ya utafiti huu yanazidi kuonyesha kuwa waalimu wa shule binafsi za Kikristo wameridhika kwa kiasi kikubwa mno na mazingira ya kazi ya shule zao kuliko waalimu wa shule za serikali na shule binafsi zinazomilikiwa na watu binafsi. Hali hii, kwa kiasi fulani, huonyesha kwa nini wanafunzi wa shule binafsi za Kikristo hufaulu vizuri mno kitaaluma kuliko wale wa shule za serikali na shule nyingine za watu binafsi.

iv) Waalimu walio wengi katika shule za serikali, shule za Kiislamu na shule za watu binafsi waliona kuwa uongozi wa shule zao ulifanya kazi kwa ufanisi mdogo sana. Zaidi ya hayo, waalimu walioona kuwa uongozi wa shule zao ulifanya kazi kwa ufanisi mkubwa walielekea kuwa na moyo wa kujitolea zaidi katika kazi ya ualimu, na matokeo yake shule zao zilifanya vizuri zaidi katika mitihani ya taifa kuliko shule ambazo waalimu wake waliona kuwa uongozi wa shule haukufanya kazi kwa ufanisi.

v) Matokeo ya uchunguzi wa majadiliano ya vikundi lengwa (matokeo ya kiubora) yanaonyesha kuwa kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu ni cha chini kupindukia. Hali hii hujitokeza zaidi kwa waalimu wa shule za serikali na shule za watu binafsi. Matokeo haya yanaonyesha kuwa, kwanza, waalimu wachache tu ndio waliochagua kwa hiari yao kufanya kazi ya ualimu na kwamba mazingira duni ya kazi yaliyopo katika shule nyingi za serikali na mishahara midogo wanayoipata husaidia tu kuonyesha na kusisitiza jinsi waalimu hao wasivyoipenda kazi ya ualimu. Athari za kiwango kidogo cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu ni kubwa mno na zinaonekana bayana kwa kuwepo matokeo mabaya ya wanafunzi kitaaluma katika shule za serikali na za watu binafsi. Zaidi ya hayo, kiwango kidogo cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu kwa kiasi fulani kinaweza kuonyesha msuguano mkubwa uliopo miongoni mwa waalimu.

vi) Matokeo ya utafiti huu hayaonyeshi jinsi hali ilivyo katika shule zote zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu. Mathalani, wakati kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu kilikuwa na uhusiano mkubwa na ufaulu wa wanafunzi katika shule za serikali na shule za Kikristo, hapakuwa na uhusiano wa moja kwa moja kati ya kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu na ufaulu wa wanafunzi miongoni mwa shule zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu. Hali hii inaonyeshwa na ukweli kwamba, wakati kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu katika shule hizi kilikuwa cha juu kwelikweli, ufaulu wa wanafunzi kitaaluma katika shule hizi ulikuwa duni kwelikweli. Hata hivyo, matokeo haya hayana budi kutafsiriwa kwa uangalifu kwani ukubwa wa sampuli ya waalimu katika shule za Kiislamu kwa kiasi fulani ilikuwa ndogo mno kulinganisha na shule nyingine.

vii) Utafiti huu haukuchunguza kwa kina suala la vigezo vinavyotumiwa katika kuwapangia waalimu masomo ya kufundisha, suala ambalo lilikuwa mojawapo ya malengo ya utafiti huu. Sababu kubwa ni kwamba ilidhihirika kwamba hakika waalimu hufundisha masomo waliyosomea katika vyuo vya ualimu au vyuo vikuu. Hivyo, kigezo kikuu kilichotumiwa na wakuu wa shule kuwapangia waalimu masomo ya kufundisha ni kwamba mwalimu anatakiwa kuwa amesoma somo hilo chuoni.

4.2 Hitimisho na Mapendekezo

Utafiti huu umeonesha mambo makuu matatu kuhusiana na waalimu ambayo huchangia/kuamua ufaulu wa wanafunzi kitaaluma, nayo ni sifa za walimu kitaaluma, kujituma na moyo wao wa kujitolea kwa kazi ya ualimu na mtazamo walio nao kuhusu ufanisi wa uongozi wa shule. Pindi waalimu wanapokuwa na moyo wa kujitolea na mtazamo chanya kuhusu uongozi wa shule, wanafunzi huelekea kufanya vizuri zaidi katika kazi zao za kitaaluma.

Hata hivyo, ukiacha shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kikristo, matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu ni cha chini sana na kwamba waalimu walio wengi wanaona uongozi wa shule zao kuwa ni duni na usiofanya kazi kwa ufanisi. Kiwango duni cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu na uongozi mbaya wa shule kwa kiasi fulani husababisha wanafunzi wa shule nyingi nchini kufanya vibaya kitaaluma.

Kwa kuzingatia hitimisho hili, mapendekezo yafuatayo yanatolewa kwa lengo la kuboresha kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu, na vilevile ufanisi wa uongozi wa shule, ambapo matokeo yake kufanya hivyo kunaweza kuleta manufaa katika ufaulu wa wanafunzi kitaaluma na kubadilisha hali duni ya matokeo ya mitihani ya taifa ya kidato cha nne. Mapendekezo haya yamefikiwa kutokana na matatizo yanayojitokeza katika matokeo hayo, na vilevile kutokana na maoni ya washiriki kuhusu namna ya kuboresha kiwango cha elimu nchini.

i) Kujituma na moyo wa kufanyakazi walio nao waalimu umejitokeza kama tatizo kuu linaloathiri ufaulu wa wanafunzi kitaaluma, huku waalimu walio wengi, hususan katika shule za serikali, wakionyesha kuwa na kiwango cha chini sana cha moyo wa kujitolea kwa kazi ya ualimu. Kiwango hiki kidogo sana cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu kinasababishwa zaidi na malipo duni na mazingira duni ya kazi katika shule na kile ambacho waalimu wanakiita ‘serikali kutojali’ kazi ya ualimu. Ili kuinua moyo wa kujitolea wa waalimu kwa kazi ya ualimu, hatua zifuatazo hazina budi kutiliwa maanani:

a. Serikali na wadau wengine wanapaswa kushughulikia kwa dhati tatizo la mazingira duni ya kazi wanayokabiliana nayo waalimu, ikiwa ni pamoja na tatizo la makazi, huduma za jamii kama vile maji na umeme.

b. Suala la malipo duni lilijitokeza kama tatizo kubwa katika kuvutia waalimu kujiunga na kuendelea na kazi ya ualimu. Mishahara ya waalimu bado ni midogo mno kiasi cha kusikitisha. Ikumbukwe kwamba utafiti huu na tafiti nyingine nyingi zimeonyesha kila mara kwamba malipo duni ndiyo sababu inayowakatisha tamaa sana waalimu. Hivyo basi, tatizo hili halina budi kushughulikiwa kama tatizo la dharura iwapo tunataka kuboresha kiwango cha elimu na kubadilisha hali duni ya matokeo ya mitihani ya taifa. Sambamba na kuboresha malipo ya waalimu, suala la kuwapandisha waalimu madaraja kwa wakati halina budi kushughulikiwa kwa kupunguza urasimu usio wa lazima katika mchakato huo. Kwa sasa waalimu wengi wamefanywa kuamini kuwa kupandishwa daraja ni suala la wateule wachache, badala ya kuwa suala la stahili ya mwalimu kulingana na sifa njema alizo nazo.

c. Tunapaswa kuwa na viwango vya chini kabisa vinavyokubalika vya shule kuitwa shule. Kwa sasa, kuna tofauti kubwa sana miongoni mwa shule, kwani kuna zile zinazohangaika hata kupata chaki na shule zenye vifaa vya kutosha kama vile maktaba na maabara. Programu zetu za elimu ambazo zinaonesha kwa muda mrefu mno zimekuwa zikijishughulisha zaidi na idadi hazina budi kupitiwa upya na kutilia maanani zaidi suala la kuongeza ubora.

d. Ni muhimu kuwa na taratibu za kuwatambua na kuwatuza waalimu wanaofanya kazi kwa kiwango kizuri sana kuzidi wengine. Kwa sasa, juhudi za ziada za waalimu hazitambuliwi wala kutuzwa. Wakati wa majadiliano ya vikundi lengwa, waalimu wengi walilalamika kwamba wanafunzi pekee ndio wanaotambuliwa na kutuzwa pindi wanapofaulu vizuri sana. Lakini tunaelekea kusahau kwamba kwa kila mwanafunzi anayefaulu vizuri sana, kuna mwalimu aliyefanya juhudi zaidi kumwezesha kufaulu, na juhudi hizi hazina budi kutambuliwa na kutuzwa ipasavyo.

e. Ni suala muhimu sana kwenye kazi ya ualimu, walimu wenyewe wakifahamu kikamilifu Sera ya Elimu na Mafunzo na maelekezo/maagizo mengine yote na program/mipango inayotolewa na viongozi ngazi za juu kuletwa kwao. Walimu kuzielewa sera na mipango ni muhimu sana ili wazitekeleze vyema na kwa tija, hatimaye waboreshe ufanisi wa sekta ya elimu na uwajibikaji

f. Mchakato wa kudahili wanafunzi wanaokwenda kujiunga na kozi ya ualimu tarajali vyuoni kuna haja ya kuupitia upya na kuuboresha. Tanzania inahitaji watu ambao si tu wana shauku ya kufundisha bali wawe na nia thabiti na uwezo wa kufundisha kwa ufanisi. Vigezo vya kudahili wanafunzi wanaokwenda kusomea ualimu na kufundisha vinapaswa kuwa sawa kwa wale waliofaulu vizuri tu masomo yao ngazi za sekondari kama ilivyo kwa wanaochukuliwa kusomea udaktari na sheria. Kushindwa kufanya hivyo tutaendelea kudhoofisha ubora wa elimu na maendeleo katika nchi yetu.

g. Maadili kwa Walimu, kujituma uwajibikaji na uaminifu ni muhimu sana katika kurejesha hadhi na thamani ya taaluma yao kwa ujumla. Walimu wakumbuke kuwa wamebeba jukumu kubwa la maendeleo ya Tanzania na wana mchango wa kipekee kwenye kujenga mustakabli na mwelekeo wa nchi yetu. Walimu wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwenye jamii na kwenye taaluma yao.

h. Walimu kufahamu haki zao na kusubiri wengine kuzitetea na kuzilinda hakutoshi, ni lazima wajipange na kuchukua hatua kamili na za uhakika bila kukata tamaa hadi watakapoona haki zao zimetekelezwa, huku wakihakikisha wanawajibika kwa viwango kubalifu kwa jamii.

ii) Ili kuboresha utendaji kazi wa waalimu kitaaluma, kuna haja ya kufufua programu endelevu za mafunzo kazini kwa waalimu. Kwa sasa, programu hizi ni adimu, nazo hutolewa mara moja moja huku zikiwa na nguvu ndogo ya kuboresha weledi wa waalimu. Hapana budi vilevile kuwa na programu za mara kwa mara za mafunzo ya uongozi wa shule kwa sababu utafiti huu umeonesha kuwa waalimu wengi katika shule nyingi wanasikitishwa sana na uongozi wa shule zao, jambo ambalo hatimaye huathiri moyo wa kujitolea walio nao na hamasa yao ya kufundisha.

iii) Misingi duni ya kitaaluma ya wanafunzi ilijitokeza kama mojawapo ya sababu kuu za kuongezeka kwa kiwango cha wanafunzi waliofeli katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne. Katika baadhi ya shule, hali ilishtua kwa kiasi fulani kubaini kuwa baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari hawakujua kuandika! Hivyo basi, kuna haja ya kuchunguza tena mwenendo wa Mtihani wa Darasa la Saba na pengine kufikiria kuimarisha Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili kwa kurejesha tena viwango vya kufaulu mtihani huo.

iv) Utafiti huu ulitumia sampuli ndogo tu ya shule zilizochaguliwa kwa kufuata utaratibu maalumu badala ya kuzichagua kiholela. Hakika, baadhi ya vipengele vya shule kama vile shule za Kiislamu viliwakilishwa vibaya kwani idadi ndogo tu ya shule ndiyo iliyoshiriki. Kwa sababu hiyo, majumuisho kuhusu matokeo haya hayana budi kufanywa kwa tahadhari na umakini sana.

v) Utafiti huu umechunguza kiwango cha kujituma na moyo wa kujitolea katika kazi miongoni mwa waalimu. Ili kufanya ulinganifu, tafiti zitakazofuatia hazina budi kulenga namna ya kupata kiwango cha kujituma, nia ya kufanya kazi na moyo wa kujitolea miongoni mwa walimu na taaluma nyingine ili kuoanisha matokeo ya utendaji kwa ujumla.

Marejeo

Caprara, G.V., Barbaranelli, C., Steca, P. & Malone, P.S. (2006). Teachers’ self-efficacy beliefs as determinants of job satisfaction and students’ academic achievement: A study at the school level. Journal of School Psychology, 44, 473-490.

Ministry of Education and Vocational Training (MoEVT, June 2010). Secondary Education Development Programme II (July 2010-June 2015).

Mosha, H.J. (1988). A reassessment of the indicators of primary education quality in developing countries: Emerging evidence from Tanzania. International Review of Education, 17-45.

Mosha, H.J. (2011). The state of quality of education in Tanzania: A candid reflection. Makala iliyowasilishwa katika Kongamano la Elimu, Dar es Salaam (Juni 2011).

National Examinations Council of Tanzania (NECTA, 2011). Examination results – Statistics for October 2010 results.

Oduro, G.K.T., Dachi, H., & Fertig, M. (2008). Educational leadership and quality education in disadvantaged communities in Ghana and Tanzania. Makala iliyowasilishwa kwenye Mkutano wa Baraza la Jumuiya ya Madola la Uongozi na Usimamizi wa Elimu, Durban, Afrika Kusini (Septemba 2008).

Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (wa 61, Oktoba 2006). Wazungumzaji wanasisitiza umuhimu wa elimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya kijamii, Taarifa kwa Vyombo vya Habari, Inapatikana katika intaneti: http://www.un.org/News/Press/docs/2006/gashc3847.doc.htm

Uwezo (2010). Are our children learning? Annual Learning Assessment Report Tanzania 2010. Dar es Salaam: Uwezo, TENMET & Hivos/Twaweza.


[1] Shule zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu ziliondolewa katika uchambuzi huu kutokana na idadi ndogo sana ya shule hizo katika sampuli hii. Shule moja tu ndiyo iliyokuwa na sifa za kujumuishwa katika uchambuzi wa mwisho.

[2] Shule zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu ziliondolewa katika uchambuzi huu kutokana na idadi ndogo sana ya shule hizo katika sampuli hii. Shule moja tu ndiyo iliyokuwa na sifa za kujumuishwa katika uchambuzi wa mwisho.

[3] Ikumbukwe kuwa waalimu 11 tu kutoka shule moja ya Kiislamu ndio waliounda sampuli hii.

[4] Kwa mara nyingine, ikumbukwe kwamba waalimu 11 tu kutoka shule moja tu ndio waliounda sampuli ya shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu.

[5] Data kuhusu waalimu wa shule za Kiislamu hazina budi kuchambuliwa kwa uangalifu kwani sampuli yao iliundwa na washiriki wachache tu.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More