Monday, February 21, 2011

Serikali Yatangaza Ajira 9,226 Kwa Walimu wa Sekondari na Vyuo Nchini


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa (kati) akitangaza ajira kwa waalimu
--
Katika mwaka wa masomo 2009/10 jumla ya wanafunzi 19,652 walihitimu mafunzo ya ualimu wakiwemo ngazi ya shahada 12,120 na stashahada 7,532. Kati ya wanafunzi hao jumla ya wanafunzi 17,684 walihitimu na kufaulu masomo yao, wenye shahada wakiwa 12,095 na wenye stashahada 5,589.

Uchambuzi wa sifa za wahitimu 17,684 waliohitimu na kufaulu mitihani yao umeonesha kuwa jumla ya wahitimu 8,857 wametoka kazini (in-service). Idadi hiyo inajumuisha wenye shahada 7,437 (25 kutoka Zanzibar) na wenye stashahada 1,420. Walimu hao wamerudi kwa waajiri wao ili wapangiwe kazi kulingana na elimu yao. Aidha, kuna wahitimu 328 kutoka Zanzibar (wakiwemo 303 tarajali na 25 kutoka kazini) ambao wanatarajiwa kuajiriwa katika shule na vyuo vya Zanzibar. Hivyo, wahitimu wanaobakia ambao wamepangwa kufundisha katika shule za sekondari na vyuo vya ualimu Tanzania Bara ni 8,524 wakiwemo wenye shahada 4,355 na wenye stashahada 4,169.

Kama ilivyobainishwa katika sehemu ya kwanza ya taarifa hii, jumla ya wahitimu 8,524 waliohitimu na kufaulu mitihani yao wataajiriwa na Serikali katika mwaka huu wa fedha. Vilevile Serikali imekubali kuajiri walimu 702 (wakiwemo 565 wenye shahada na 137 wenye stashahada) waliomaliza mafunzo yao miaka ya nyuma ambao wameomba kuajiriwa Serikalini.
Hivyo, jumla ya walimu wote watakaoajiriwa Serikalini kwa mwaka wa fedha 2010/2011 ni 9,226 wakiwemo wenye shahada 4,920 na wenye stashahada ni 4,306. Kati ya walimu watakaoajiriwa jumla ya walimu 9,039 wamepangwa kufundisha katika shule za sekondari na walimu 187 wamepangwa kufundisha katika vyuo vya ualimu.

Walimu wote wa shule za sekondari wamepangwa katika Halmashauri mbalimbali kwa kutumia kigezo cha upungufu wa walimu katika Halmashauri husika. Hivyo, kila mwalimu anatakiwa kuripoti katika Halmashauri aliyopangwa kwa kuwa fedha za mshahara wake zimekasimiwa kwenye Halmashauri alikopangwa na si vinginevyo. Orodha ya walimu hao na Halmashauri walikopangwa zimetumwa kwenye Mikoa na Halmashauri. Aidha, orodha hiyo inapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi www.moe.go.tz na tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa www.pmoralg.go.tz.

Walimu wote wapya wanaagizwa kuhakikisha kwamba wanaripoti katika Halmashauri/ Vyuo vya Ualimu walikopangwa ifikapo tarehe 24/01/2011. Watendaji na wasimamizi wa elimu kwenye Halmashauri na Vyuo vya Ualimu watakuwepo kuwapokea.
Mwalimu yeyote atakayeshindwa kuripoti kwenye Halmashauri / Chuo alikopangwa baada ya siku saba (7) tangu tarehe anayotakiwa kuripoti atahesabika kuwa amekataa kukubali nafasi ya ajira aliyopewa na Serikali.

Baada ya kuripoti kwenye Halmashauri/Vyuo waajiri watatakiwa kuwajazia walimu hao Fomu maalum zenye Taarifa ya Kiutumishi ya Mtumishi (Personal Data Form)na kuziwasilisha Ofisi ya Rais, UTUMISHI pamoja na barua ya ajira ya mtumishi. Taarifa hizo zikiwa katika “hard” na “soft copy” ziwasilishwe UTUMISHI kabla au ifikapo tarehe 29/01/2011 ili watumishi hao waingizwe katika mfumo wa malipo (Payroll). Waajiri wanakumbushwa kwamba “Computer Data Sheet” hazitahitajika katika zoezi hili.

Waajiri(Wakurugenzi wa Halmashauri na Katibu Mkuu–Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi)watawalipa malipo stahili kwa mujibu wa nyaraka na miongozo ya Serikali kuhusu waajiriwa wapya.

Nawatakia utumishi mwema katika Sekta ya Elimu.

Imetolewa na:

MHE. DKT.SHUKURU J. KAWAMBWA
WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

1 comments:

issue siyo ajira, serikali inapaswa kuwalipa vilevile. Kuajiri walimu wengi bila mishahara ni kutwanga maji kwenye kinu

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More