Friday, November 23, 2012

Utafiti: Uelewa finyu wa mitaala chanzo cha matokeo mabaya ya mitihani


 Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dr Kitila Mkumbo 
akitoa matokeo ya utafiti katika ukumbi wa mikutano wa HakiElimu.
 Imebainika kuwa matokeo mabaya kwenye mitihani ya taifa hayahusiani na kutofautiana kati ya mitihani na maudhui ya mtaala ingawa, uelewa finyu wa walimu juu ya maudhui ya mtaala wa elimu ndicho chanzo cha matokeo mabovu ya mitihani ya taifa.

Pia imebainika kuwa mtaala wa elimu unatekelezwa kwa kiwango duni kwa kuwa idadi kubwa ya walimu hawaelewi mahitaji ya mtaala na mazingira ya kufundishia na kujifunzia ni duni katika utekelezaji bora wa mtaala.
Hayo yamo katika ripoti mpya ya utafiti uliofanywa na HakiElimu kwa kushirikiana na Dr Kitila Mkumbo wa chuo kikuu cha Dar es Salaam wenye kichwa cha habari 'Uhusiano kati ya Mitihani na Mitaala,' utafiti huo ulikuwa na lengo la kujibu swali Kuu: Je, Wanafunzi Wanafeli Mitihani au Mitihani Inawafelisha Wanafunzi?

Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya HakiElimu, Marjorie Mbilinyi 
akifuatilia ripoti ya utafiti iliyozinduliwa leo HakiElimu
"matokeo duni katika mtihani wa taifa yanatokana utekelezaji duni wa mtaala kuliko mitihani yenyewe, Inaonekana kwamba, japokuwa Serikali imekuwa ikitekeleza mtaala unaomjengea mwanafunzi ujuzi tangu 2005, ni walimu wachache wanaoifahamu dhana na falsafa ya mtaala huu"Alisema Dr Mkumbo

Utafiti huo umezidi kubainisha kuwa ingawa maudhui ya mtaala wa elimu yanaonekana kuwa ni yale ya kumjengea mwanafunzi ujuzi, taratibu za tathmini hazifuati falsafa hiyo. Kwa mujibu wa mtaala wa elimu, mazoezi na maendeleo ya kawaida ya shuleni yanatakiwa kuchangia asilimia 50 za alama ufaulu na asilimia 50 ndio zinatoka kwenye mtihani wa mwisho suala ambalo utafiti umelitilia mashaka kwani hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa baraza la mitihani linatumia falsafa hiyo.

"Falsafa mojawapo ya mitaala inayozingatia ujuzi na uwezo wa mhitimu ni kutoa kipaumbele kilichosawa kati ya mitihani ya mwisho na mitihani ya mashuleni, Kulikuwa na taarifa za kukanganya kuhusu mchango wa mazoezi kwenye alama ya mwisho ya mwanafunzi" alisema Mkumbo.

Ripoti hiyo ilizidi kueleza kuwa mmoja wa maafisa wa mtihani aliyesailiwa alisema waziwazi kuwa mazoezi yanachangia nusu ya alama za mwanafunzi katika mtihani wa mwisho, walimu walikuwa hawaamini kama hali ndivyo ilivyo. Walimu walieleza kuwa iwapo alama za kwenye mazoezi zingetumiwa kwenye mtihani wa mwisho, kusingekuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofeli mtihani kama tulivyoshuhudia hivi karibuni katika mfumo wetu wa elimu.
Meneja katika idara ya utafiti na uchambuzi wa sera wa HakiElimu Boniventura Godfrey 
akifafanua jambo.Kushoto ni Meneja wa idara ya habari na utetezi Ndugu Nyanda Shuli

Meneja wa idara ya utawala na fedha Daniel Luhamo akiwa na Mwenyekiti 
wa bodi ya HakiElimu Bi Illuminata Tukai wakifuatilia matokeo ya utafiti

Kwa miaka mitano mfurulizo hasa miaka ya 2010 na 2011 ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne katika mitihani ya taifa alishuka kwa kiwango cha kutisha kwa wanafunzi wengi zaidi ya asilimia 80 wakipata daraza la nne na sifuri. Mfano katika wanafunzi 354042 waliofanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka 2010, wanafunzi 117,021walipata daraja sifuri ikiwa ni asilimia 50 ya watahiniwa wote, wanafunzi 136,633 ambao ni asilimia 38.6 walipata daraja la nne na kufanya asilimia 88.6 ya watahiniwa wote kupata daraja la nne na sifuri. ni wanafunzi 15,335 sawa na asilimia 4.3 ndio waliopata daraja la kwanza na la pili.









0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More