Monday, November 26, 2012

Ukata unachangia uelewa finyu wa maudhui ya mtaala kwa walimu

Mkurugenzi wa Utafiti, Habari na Machapisho wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) 
Makoye Wangeleja akisisitiza jambo siku ya uzinduzi wa ripoti ya Utafiti
 Juu ya Uhusiano Uliopo Kati ya Mitihani na Mitaala


Imeelezwa kuwa ufinyu wa bajeti umekuwa ukikwamisha juhudi za kutoa elimu ya mitaala kwa walimu ili kuwajengea uwezo wa kuweza kuelewa maudhui yaliyomo kwenye mitaala ili kuwawezesha kuelewa na kuweza kutafsiri kwa vitendo maudhui ya mitaala katika ufundishaji.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Utafiti, Habari na Machapisho wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) Makoye Wangeleja wakati akichangia ripoti ya utafiti iliyowasilishwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dr Kitila Mkumbo.

Wangeleja alisema TIE imekuwa ikishirikisha walimu kwa kiasi kidogo hali inayotokana na kutokuwa na fedha za kutosha kwaajili ya kazi ya kuwashirikisha walimu katika utungazi na kuwafundisha ili kuelewa vyema maudhui ya mtaala unaotumika.
 

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti iliyofanywa na HakiElimu iliyofanya kwa ushirika wa Dr Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilieleza kuwa kwa mujibu wa mtaala wa elimu wa mwaka 2005 unaotumika sasa, mazoezi ya mwanafunzi shuleni yanatakiwa kuchangia nusu ya alama za mwanafunzi katika mtihani wa mwisho, lakini walimu hawaamini kama hali ndivyo ilivyo. 

Walimu walisema waziwazi kuwa iwapo alama za kwenye mazoezi zingetumiwa kwenye mtihani wa mwisho, kusingekuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofeli mtihani kama tulivyoshuhudia hivi karibuni katika mfumo wetu wa elimu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya utafiti, idadi kubwa ya walimu hawana uelewa wa mahitaji ya mtaala na mazingira ya kufundishia na kujifunzia ni duni katika utekelezaji bora wa mtaala.Hali ambayo Wangeleja amesema inasababishwa na ufinyu wa bajeti katika kutekeleza mpangowa kutoa elimu ya mitaala kwa walimu wote nchini.

Utafiti huo umezidi kubainisha kuwa ingawa maudhui ya mtaala wa elimu yanaonekana kuwa ni yale ya kumjengea mwanafunzi ujuzi, taratibu za tathmini hazifuati falsafa hiyo. Kwa mujibu wa mtaala wa elimu, mazoezi na maendeleo ya kawaida ya shuleni yanatakiwa kuchangia asilimia 50 za alama ufaulu na asilimia 50 ndio zinatoka kwenye mtihani wa mwisho suala ambalo utafiti umelitilia mashaka kwani hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa baraza la mitihani linatumia falsafa hiyo.

Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya HakiElimu, Marjorie Mbilinyi 
akifuatilia ripoti ya utafiti iliyozinduliwa leo HakiElimu.Pembeni ni Meneja wa Idara ya Utawala na Fedha ya HakiElimu Daniel Luhamo
"Falsafa mojawapo ya mitaala inayozingatia ujuzi na uwezo wa mhitimu ni kutoa kipaumbele kilichosawa kati ya mitihani ya mwisho na mitihani ya mashuleni, Kulikuwa na taarifa za kukanganya kuhusu mchango wa mazoezi kwenye alama ya mwisho ya mwanafunzi" alisema Dr Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha ripoti ya utafiti huo mbele za wandishi wa habari..

Kwa miaka mitano mfurulizo hasa miaka ya 2010 na 2011 ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne katika mitihani ya taifa alishuka kwa kiwango cha kutisha kwa wanafunzi wengi zaidi ya asilimia 80 wakipata daraza la nne na sifuri. Mfano katika wanafunzi 354042 waliofanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka 2010, wanafunzi 117,021walipata daraja sifuri ikiwa ni asilimia 50 ya watahiniwa wote, wanafunzi 136,633 ambao ni asilimia 38.6 walipata daraja la nne na kufanya asilimia 88.6 ya watahiniwa wote kupata daraja la nne na sifuri. ni wanafunzi 15,335 sawa na asilimia 4.3 ndio waliopata daraja la kwanza na la pili.





0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More