Tuesday, September 18, 2012

Mtihani Mpya Darasa la Saba Haumchuji Anayejua Kusoma au Asiyejua - Walimu


Na Joachim Mushi, Thehabari.com

WAKATI wanafunzi wa darasa la Saba wakitarajia kuanza mitihani yao kesho baadhi ya walimu wa Sekondari wametoa angalizo kuwa mfumo mpya unaotarajiwa kutumika kwa usaishaji huenda ukapitisha (faulisha) wanafunzi wasio na sifa hivyo kuongeza idadi ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kuingia sekondari.

Wakizungumza na Mtandao wa Thehabari.com hivi karibuni walisema mfumo huo wa usaishaji kwa kutumia mashine unaomtaka mwanafunzi kuweka kivuli kwenye jibu sahihi baada ya kuchagua ni rahisi kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa kuibia kwa jirani yake kimazingira jambo ambalo ni hatari kulingana na mazingira ya vyumba vya mitihani.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitopeni, Mjini Korogwe, Theodolph Karigita alisema mazingira ya vyumba vingi vya mitihani kwa shule za msingi ni rahisi kuibia kutokana na wanafunzi kusongamana kwenye vyumba vya mitihani, jambo ambalo kwa aina ya mtihani unaofanyika upo uwezekano wa kupata wanafunzi wasiokuwa na sifa kuingia kidato cha kwanza.Mwalimu Karigita alisema kibaya zaidi kwa sasa hadi mtihani wa hisabati utafanyika kwa wanafunzi kuchangua yaani jibu sahihi kati ya A, B, C au D kabla ya kuweka kivuli kwenye jibu sahihi eneo, kitendo ambacho itakuwa rahisi kwa wasiojiweza kuangalia kwa mwanafunzi aliyejirani naye.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Boma ya Mjini Korogwe mkoani Tanga, Amir Nassoro alisema mtihani kama huo hauwezi kumpima mtoto kwamba anajua kusoma ama kuandika bali unaweza kujikuta unapitisha hata wale wasiokuwa na sifa kulingana na mazingira yetu. "Hivi unampimaje mtoto asiyejua kusoma na kuandika kwa kuchagua jibu sahihi au lisilokuwa sahihi...eneo kama hili hata asiyejua anaweza kubahatisha kwa kuandika A tu au B na hata C tu," alisema Nassoro.

Mwalimu Nassoro alitolea mfano kuwa mwaka 2010 alifanya utafiti mwepesi kwa kutunga mtihani wa kuchagua shuleni hapo na kuwapa wanafunzi kwa maelekezo kuwa baadhi waandike A tu na wengine B na vivyo hivyo kwa majibu mengine, lakini ilionekana wapo baadhi walifanikiwa kufanya vizuri bila ya kujua alichokichagua ni jibu sahihi.

"Katika mazingira kama hayo huwezi kumpima mwanafunzi wakati mtihani anaofanya haumchuji anayejua kusoma au asiyejua..." alisema mwalimu Nassoro.*Habari hii imeandaliwa na Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na HakiElimu

 

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More