Wanafunzi wa darasa la saba nchini kote kesho na keshokutwa wanatarajia kuanza mitihani ya kumaliza elimu yao ya msingi ambapo kwa mara ya kwanza tekinolojia mpya iitwayo Optical
Mark Reader (OMR) itatumika.
Watahiniwa watatumia fomu maalum za OMR kujibia
mtihani na majibu yao yatasahihishwa kwa kutumia kompyuta. Masomo yatakayotahiniwa katika mtihani huo ni
Kiswahili, English Language, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.
Jumla ya wanafunzi 894,881 wamesajiliwa kufanya mtihani huo ambapo wavulana ni 426,285 sawa na asilimia 47.64 na wasichana ni 468,596 sawa na asilimia 52.36. Aidha, kati
ya wanafunzi hao, wapo wanafunzi 874,379 watakaofanya
mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na wanafunzi 20,502 watafanya kwa
lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo waliyoitumia kujifunzia. Wanafunzi wasioona waliosajiliwa kufanya
mtihani ni 92 wakiwemo wavulana 53 na wasichana 39. Watahiniwa wenye uono hafifu ambao huhitaji
maandishi makubwa ni 495, kati
yao wavulana ni 238 na wasichana ni 257.
Mwaka jana, watahiniwa 1,010,619 waliandikishwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2011 ambapo jumla ya watahiniwa 993,324 waliandikishwa kufanya mtihani kwa
lugha ya Kiswahili na watahiniwa 17,295 waliandikishwa kufanya mtihani kwa lugha ya Kingereza
ambayo walikuwa wakiitumia katika kujifunzia.
HakiElimu inawaasa wanafunzi, walimu na wadau wote kuzingatia misingi bora katika kipindi chote cha mitihani ya kumaliza elimu ya msingi ikiwa ni daraja moja muhimu linalotakiwa kuwavusha wanafunzi kutoka elimu ya msingi na kuingia elimu ya sekondari.
Kila la heri wanafunzi wote katika mitihani yenu.
0 comments:
Post a Comment