Thursday, September 27, 2012

HakiElimu yazindua kampeni ya kuhamasisha uboreshaji wa Elimu ya Awali

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Awali ya Mchangani iliyopo jijini Dar es Salaam 
wakionesha bango lenye ujumbe juu ya maboresho ya elimu ya awali.
Baadhi ya walimu na wafanyakazi wa Taasisi ya HakiElimu wakionesha mabango 
mbalimbali kwa wanahabari kuhamasisha elimu ya awali.

Baadhi ya walimu na wafanyakazi wa Taasisi ya HakiElimu wakionesha 
mabango mbalimbali kwa wanahabari kuhamasisha elimu ya awali.
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia, 
akisoma taarifa kuzindua kampeni hizo.

TAASISI ya HakiElimu leo imezindua kampeni ya kuhamasisha jamii na Serikali juu ya umuhimu wa elimu ya awali kwa watoto kabla ya kujiunga na darasa la kwanza.
Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika Ofisi za HakiElimu na kuhudhuriwa na baadhi ya walimu na wanafunzi wa awali, waandishi wa habari, wadau mbalimbali wa sekta ya elimu, pamoja na taasisi za malezi na makuzi ya watoto.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia alisema shirika hilo lemeamua kuzindua kampeni hiyo iliyopewa jina la “Boresha Elimu ya Chekechea” lengo kuu likiwa ni kuitaka Serikali itimize ahadi na wajibu wake wa kutoa elimu bora kwa wanafunzi wote wa elimu ya awali.
Mkurugenzi huyo alisema elimu ya awali kwa mtoto ni muhimu sana katika kujenga msingi imara kielimu na endapo elimu hiyo itatolewa kikamilifu, inakuwa ni msingi imara kwa mtoto katika elimu yake ya baadae na pia elimu hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya mtoto kimwili, kiakili na kimaadili.




Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia, akigawa zawadi ya vifaa anuai 
vya masomo kwa wanafunzi wa shule ya awali ya Mchangani mara baada ya uzinduzi huo.


Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia (mwenye blauzi nyekundu) 
akigawa zawadi ya vifaa anuai vya masomo kwa wanafunzi wa shule ya awali ya Mchangani 
mara baada ya uzinduzi huo

Wageni waalikwa katika hafla ya uzinduzi wa campaign hiyo
“Katika Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 1995 Serikali inaonesha umuhimu wa elimu ya awali, inapotamka; ‘Tafiti kadhaa zilizofanyika nchini katika miaka ya 1980 zilibaini kuwa watoto waliopitia elimu ya awali huwa na mafanikio makubwa zaidi wanapoanza darasa la kwanza. Kutokana na kutambua umuhimu huu, Serikali iliamua kuingiza Elimu ya Awali kwa watoto wenye umri wa miaka 5 na 6 kwenye mfumo rasmi wa elimu na kila shule ya msingi inapaswa kuwa na madarasa ya Elimu ya Awali’,” alisema Missokia.
Alisema kabla ya uzinduzi wa kampeni hii HakiElimu imefanya tafiti katika sehemu mbalimbali nchini na kubaini hali ya utoaji wa elimu ya awali na mazingira yake inatia huruma kwani elimu hiyo inavyotolewa katika mazingira yasiyofaa jambo ambalo linachangia kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.

“Kama ilivyo katika elimu ya msingi na ile ya sekondari, elimu ya awali imegubikwa na changamoto nyingi. Baadhi ya changamoto hizi ni upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, unaosababisha mrundikano mkubwa katika madarasa, ukosefu mkubwa wa walimu wenye taaluma ya elimu ya awali pamoja na vifaa vya kufundishia. Aidha, kutokuwepo na tofauti ya kimadarasa katika elimu ya awali (yaani watoto wa umri wa miaka 5 na miaka 6 kusoma katika darasa moja), na wingi wa masomo pia ni changamoto,” alisema.
Aidha aliongeza kuwa licha ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, katika makadirio na matumizi ya wizara yake ya mwaka 2012/13, kukiri kuwa Serikali imetoa mwongozo kwa kila shule ya Msingi kuwa na darasa la Elimu ya Awali, lenye madawati yanayolingana na hali ya watoto wa elimu hiyo, kujenga vyoo kwa ajili ya watoto wa Elimu ya Awali wasiingiliane na wale wa shule za msingi, lakini bado kuna mapungufu makubwa katika utekelezaji wake.

“Baada ya kuona madhara ya kukosa elimu bora ya awali kwa watoto wetu, HakiElimu inatoa wito kwa watanzania wote nchini wenye mapenzi mema na maendeleo ya taifa letu kuungana nasi katika kampeni hii kwa njia zifuatazo; Kuhimiza wananchi wote wenye watoto wenye umri wa kuandikishwa shule za awali wafanye hivyo kwa wingi. Kuna baadhi ya sehemu inaripotiwa wazazi bado hawajaelewa umuhimu wa kuwapeleka watoto katika madarasa haya ya awali.

“Kuwabana viongozi wetu tuliowachagua kuanzia mwenyekiti wa mtaa, diwani na Wabunge wetuwanachukua hatua kukabiliana na changamoto zilizopo ili kufanikisha Elimu bora ya Awali kwa watoto wetu.
Wananchi kuandika barua kwenye magazeti mbalimbali hapa nchini zikielezea hali ya elimu ya awali inavyotolewa katika maeneo mliyopo.”

HakiElimu imeshauri barua zinazoandaliwa na wananchi kuzituma moja kwa moja kwa Wahariri wa magazeti wanayoyasoma kupitia anuani zilizopo katika gazeti husika, au wanaweza kuzituma kupitia sanduku la barua 79401 Dar es Salaam zikiwa na kichwa cha habari ‘BORESHA CHEKECHEA’, ambapo HakiElimu itafanya kazi ya kuzipeleka katika magazeti mbalimbali nchini.

Aidha, ili kuchagiza mafanikio katika sekta ya elimu, HakiElimu imeandaa vipindi vya radio katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Tabora, Tanga, Kagera, Dodoma na Mara ambavyo vitatoa nafasi ya Marafiki wa Elimu kujadili jinsi gani elimu ya awali inaweza kuboreshwa.

Pamoja na kampeni hiyo, HakiElimu imezindua matangazo mapya mawili ya redio na luninga, moja likiwa linaonesha changamoto za elimu ya awali na ufundishaji wake katika shule za serikali na la pili linaloonesha mfano wa darasa bora na ufundishaji unaojitoshereza.

Hata hivyo kwa Watanzania wanaotumia mtandao wa ‘Internet’ wanaweza kushiriki kampeni hii kwa kutembelea; www.facebook.com/hakielimu, www.twitter.com/hakielimu, www.hakielimu.blogspot.com na kuangalia matangazo mapya waweza kutembelea YouTube kupitia www.youtube.com/hakielimutz.



0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More