Wednesday, August 22, 2012

Mitaala shule za msingi inawachanganya wanafunzi – Walimu

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kitopeni kutoka Wilaya ya Korogwe.
BAADHI ya walimu wa shule za msingi wilaya za Korogwe na Moshi wamelalamikia mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala kwa shule za msingi pamoja na idadi kubwa ya masomo kwa wanafunzi wa madarasa ya chini, kuwa yamekuwa yakiwachanganya wanafunzi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti hivi karibuni walisema mabadiliko ya mara kwa mara kwa mitaala yanayofanywa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi bila maandalizi yamekuwa chanzo cha vikwazo cha kufanya vizuri kwa sekta hiyo.

Akizungumza hivi karibuni na mwandishi wa habari hizi, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Gerezani, mjini Moshi, Khadija Mtui alisema mabadiliko ya mitaala ya mara kwa mara yanawachanganya wanafunzi pamoja na walimu hivyo kuwa kikwazo.

Alishauri kuwepo na maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha walimu ambao ni wadau wakubwa wa sekta ya elimu kabla ya mabadiliko ya mitaala hiyo. Alisema pamoja na hali hiyo mabadiliko ya vitabu vya masomo bila utaratibu mahususi ni tatizo pia katika mafanikio ya sekta hiyo kitaaluma.

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Lwengera Darajani, wakiwa wamapumziko
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitopeni ya Mjini Korogwe, akizungumza na mtandao wa Thehabari.com hivi karibuni.
“Mabadiliko ya mitaala na mchanganyiko wa vitabu bila utaratibu mahususi ni tatizo, kwa sasa hivi kila shule ina kitabu chake katika somo fulani…hata hivyo licha ya mabadiliko ya mara kwa mara hakuna maandalizi, mimi tangu nimalize chuo 1979 sijaenda semina yoyote wala mafunzo kujiandaa na mabadiliko ya mitaala hii. Hili linachangia pia,” alisema mwalimu Mtui.

Akifafanua zaidi Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Muungano, ya wilayani Moshi, Ashati Elihaki alisema mbali na mchanganyiko juu ya suala la vitabu vya masomo mabadiliko ya mitaala yamegeuza baadhi ya masomo kubaki kama ‘kiini macho’ jambo ambalo ni tatizo kwa walimu.

“…angalia kwa mfano somo kama la Tehama linaloanza kufundishwa darasa la tatu hadi la saba somo hili lipo kinadharia zaidi, hakuna walimu ambao wameandaliwa kufundisha somo hili lakini linatakiwa kufundishwa eti kwa kutumia mwongozo wa mwalimu kimsingi hii si sawa,” alisema Elihaki.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitopeni ya Mjini Korogwe, Theodolph Karigita alisema tofauti na ilivyokuwa hapo awali mitaala ya sasa imevurugwa kiasi kikubwa jambo ambalo linawachanganya walimu na hata wanafunzi hivyo kushindwa kufanya vizuri.

“…Mitaala imevurugwa sana, kunamchanganyiko wa masomo nadhani unakumbuka kuna kipindi baadhi ya masomo yaliunganishwa kama Jiografia, Historia na Uraia wakaita maarifa ya jamii…kipindi hiki wanafunzi walifanya vibaya sana hivyo ikabadilishwa sasa watoto wanafanya vizuri tofauti na awali,” alisema Karigita.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lwengera Darajani, Youze Mbwambo alisema idadi kubwa ya masomo kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tatu ni chanzo kingine cha wanafunzi hao kufanya vibaya kwani wamekuwa wakibebeshwa mzigo pasipo sababu za msingi.

Akizungumzia hoja hizo zilizotolewa na baadhi ya walimu, Ofisa Elimu Taaluma, Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Elius Mkwizu alisema mabadiliko yanayofanywa na wataalamu hufanywa kwa malengo mazuri licha ya kuwepo na changamoto kadhaa maeneo tofauti.

*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Taasisi ya HakiElimu.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More