Tuesday, June 5, 2012

Madiwani na kitendawili cha elimu maalumu Namtumbo
BaadhiyawanafunziwenyeulemavuwaakilikatikaShuleyaMsingiNamtumbo.Uongoziwahalmashauriyawilayahiyounalaumiwakwakutengakiasikidogo cha fedhakuendelezaelimumaalumuwilayanihumo.
Na Vicent Mnyanyika
BARAZA la Madiwani katika Wilaya ya  Namtumbo, mkoani Ruvuma linatajwa kuwa chanzo cha kuzorota kwa elimu maalumu wilayani humo.Kitendo hicho kimesababisha watoto wengi wenye mahitaji maalumu na wenye umri wa kwenda shule,  kubaki nyumbani bila kupata haki yao ya elimu.
Uchunguzi wa Mwananchi  uliofanyika hivi karibuni umebaini baraza la madiwani halitilii mkazo aina hiyo ya elimu kwa kupanga bajeti ndogo isiyorandana na mahitaji halisi ya mipango iliyoanzishwa ya kuendeleza elimu maalumu wilayani humo.
Kwa sasa Wilaya ya Namtumbo ina kitengo kimoja tu cha watoto wenye mahitaji maalumu kilichopo katika Shule ya Msingi Namtumbo  kinachohudumia wanafunzi wenye ulemavu wa akili tu. Kitengo hiki kina mwalimu mmoja na wanafunzi watano wanaohudhuria kati ya 26 walioandikishwa.
Kitengo hicho kilichoanzishwa mwaka 1997  ndicho kitengo pekee kinachoshughulika na utoaji wa  elimu kwa watoto wenye ulemavu katika wilaya nzima, huku kikishindwa kuwahudumia makundi mengine ya wanafunzi wenye ulemavu kama walemavu wa macho na wasiosikia.
Mratibu wa Elimu maalum wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo,  Joseph Chengula anasema changamoto kubwa inayozorotesha elimu maalumu katika wilaya hiyo ni bajeti ndogo inayotengwa na mamlaka husika hususan baraza la Madiwani.
“Labda kwa mwaka huu ndio kidogo imepangwa Sh milioni saba kwa ajili ya elimu maalum. Miaka mingine huwa ndogo sana,  unakuta inapangwa  milioni moja au laki tano,” anasema.
Changamoto nyingine anazozitaja ni pamoja  na upungufu wa walimu wenye utaalamu anaosema kwa sasa wapo wawili tu kwa wilaya nzima. Nyingine ni ukosefu wa miundombinu na vifaa vya kufundishia na  kujifunzia.
Takwimu za mwaka 2011 zinaonyesha kuwa, Wilaya ya Namtumbo ina jumla ya walemavu 252, kati yao wanafunzi 181 ndio wanaosoma katika shule mbalimbali kupitia  elimu jumuishi.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi hiyo inajumuisha wanafunzi 34 wenye ulemavu wa akili, wanafunzi 18 wasioona, 11 wasiosikia, walemavu wa viungo 109 na walemavu wa ngozi tisa.
 Wanafunzi 71 waliokuwa na umri wa kwenda shule hawajaandikishwa na hawapo shuleni,  wakiwamo wenye ulemavu wa akili 21, wasioona mmoja, wasiosikia  11, walemavu wa  viungo 35 na walemavu wa ngozi watatu.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo,  Kassim Ntara anasema halmashauri yake haijawahi kupewa fedha maalumu kutoka serikalini kwa ajili ya kuwahudumia wanafunzi wenye ulemavu, badala yake fedha inayotolewa anasema ni ya jumla kwa ajili ya maendeleo ya sekta za elimu, afya na huduma nyinigine.
“Hata hivyo Ntara anasema:  “Katika mwaka mpya wa fedha wa 2012/2013, halmashauri imetenga kiasi cha Sh milioni saba kwa ajili ya kitengo cha walemavu wa akili na kwamba kuna mpango wa kujenga shule moja kwa ajili ya   walemavu kama ilivyoagizwa na Serikali.”
Mwalimu pekee
Mkuu wa kitengo cha walemavu kilichopo katika Shule ya Msingi Namtumbo,  Lezile Kampango anatamani kuomba uhamisho wa kwenda wilaya nyingine,  ili aweze kuitumia taaluma yake vema,  kwani anahisi analipwa mshahara  wa bure bila ya kufanya kazi kama alivyokuwa amedhamiria.
“Natamani kuomba uhamisho kwenda mahali pengine ili elimu yangu niweze kuitumia katika mazingira bora na rafiki kwa wenye ulemavu. Hebu fikiria mimi nawafundisha wanafunzi chini ya mti, wakati wa mvua nakwenda kuwafundishia  nyumbani kwangu. Nimetoa taarifa katika ofisi ya Ofisa Elimu na mkurugenzi,  lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa,’’anasema.
Anaeleza kuwa ni dhahiri kitengo hicho kimesahaulika kwa kuwa tangu alipopangiwa hapo  mwaka 2005 hadi sasa,  kitengo hakijawahi kupata ruzuku yeyote kwa ajili ya chakula pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa watoto .
Anasema mahitaji ya msingi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu hasa wenye ulemavu wa akili ni chakula, vifaa vya kufundishia, madarasa na walimu.
“Watoto kama hawa hawawezi kusoma bila chakula, kwani mwanafunzi akihisi njaa tu anatoka nje na kurudi kwao bila hata ya kuuliza, gari ikipita wote wanatoka na kukimbilia gari. Ukiwa mwalimu inabidi uhakikishe kuna vivutio vya kutosha kuwafanya wafike shule na kukaa darasani,” anafafanua.
Kampango anaeleza kuwa mara nyingine hulazimika kuwafundisha nyumbani kwake na  kuwapatia chakula kwa gharama zake ili waendelee kusoma.
Kinachosikitisha ni kwamba wananchi na Serikali wilayani humo wameshindwa japo kujenga chumba kimoja cha daraa kwa ajili ya watoto hao, hali inayomlazimu kuwafundisha chini ya mti ama nyumbani kwake.
Ruzuku kwa wanafunzi
Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo,  Rhoda Mbilinyi  anasema mbali ya kuwa na kitengo maalumu kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa akili, wanafunzi wengine wamekuwa wakichanganywa na wanafunzi wa kawaida katika shule mbalimbali kupitia mfumo wa elimu jumuishi.
Kuhusu ruzuku anasema japo huletwa kwa kiwango kidogo, wamekuwa wakipokea fedha zinazojumuisha wanafunzi wote bila mgawanyo maalumu kwa ajili ya walemavu.
“Ni kweli wanafunzi wenye ulemavu wanahitaji mazingira rafiki,  vikiwemo vivutio. Katika kitengo cha walemavu Namtumbo kuna vivutio vichache. Wakati fulani walikuwa wanapata uji, lakini hivi sasa uchangiaji umekuwa mgumu,’’anasema na kuongeza:
 Tunahamasisha katika kipindi hiki cha mavuno waanze kuchangia na  mwaka huu katika bajeti yetu tumetenga fedha kwa ajili ya kitengo cha elimu maalumu.’’
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (Unicef ) za mwaka 2002,  zilionyeesha kuwa asilimia 98 ya watoto wenye ulemavu katika nchi zinazoendelea,  ikiwemo Tanzania hawapatiwi kabisa elimu jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wao.
Inaelezwa kuwa asilimia hii ndogo inasababishwa na kuwepo kwa shule chache maalumu kwa ajili ya watu wenye ulemavu,   ukosefu wa wataalamu, ukosefu wa vifaa na miundombinu duni isiyokidhi mahitaji  ya watu wenye ulemavu.
Aidha,  sera na sheria nyingi za nchi hizo  hazitaji moja kwa moja au kutoa utaratibu mzuri wa kutoa elimu kuhusu watu wenye ulemavu.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More