Thursday, May 10, 2012

Uhaba Wa Walimu Na Madarasa Kero kwa Wanafunzi na Walimu
Hili ni mojawapo ya madarasa ya Shule ya Msingi Selous (Darasa la Sita) Wilaya ya Namtumbo hapa wanafunzi wanaendelea na masomo.


wanafunzi wa darasa la tano wakiwa kwenye darasa la Nyasi katika shule ya msingi Selous wilayani Namtumbo


Mwalimu wa darasa la awali, Fransis Ndunguru wa Shule ya Msingi Rwinga Wilaya ya Namtumbo akiwa darasani. Darasa hili ni kibanda cha nyasi wanalotumia watoto.


Na Vicent Mnyanyika, Aliyekuwa - Namtumbo

UHABA wa vyumba vya madarasa ni moja ya changamoto kubwa inayoikabili sekta ya elimu Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma hali inayosababisha kushuka kwa kiwango cha elimu wilayani humo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni wilayani hapa baadhi ya walimu wanaofundisha katika shule za msingi wilayani Namtumbo wamesema wanatamani kuacha kazi au kuhama kutoka na changamoto nyingi zinazowakabili kwa muda bila ya kupatiwa ufumbuzi. Wanasema kuwepo kwa changamoto hizo za muda mrefu kuchangia kushusha kiwango cha elimu katika shule nyingi za mjini.
Uchunguzi uliofanywa katika shule za msingi Rwinga, Selou, Mkapa na Kidugalo zote kutoka Kata ya Rwinga umebaini shule hizo kukabiliwa na uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa hali inayowalazimu walimu kujenga vibanda vya nyasi ili kuwaepusha wanafunzi kukosa masomo kwa sababu ya uhaba huo wa madarasa. Mwandishi wa Habari na muwakilishi wa Star TV Radio Free Africa akiwa darasani akishangaa mtindo wa kuchanganya madarasa mawili katika chumba kimoja cha darasa.


Wanafunzi wa madarasa mawili wa shule ya msingi Kidugalo (Darasa la tano na la sita) wakiwa katika chumba kimoja cha darasa wakisoma kwa mtindo wa kugeuziana migongo na kufundishwa kila darasa tofauti.Njia hii inatumika sana wilayani Namtumbo ikiwa ni njia ya kukabiliana na uhaba wa vyumba vya madarasa.Shule hii ipo kilometa nne tu toka ofisi za wilaya zilipo.Hali hiyo pia imewalazimu walimu kutumia kutumia vyumba vichache vilivyopo kwa kuwachanganya wanafunzi wa madarasa mawili katika chumba kimoja hali inayotia shaka mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Mwandishi ametembelea Shule ya Msingi Kidugalo na kushuhudia zaidi ya wanafunzi 200, wa kuanzia darasa la tatu mpaka la sita wanasoma katika vyumba viwili vya madarasa huku wakiwa wamegeuziana migongo hali ambayo inachangia kushusha taaluma katika shule hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ina shule za msingi 107 kati ya hizo shule 105 zinamilikiwa na Serikali na shule mbili ni za watu binafsi na mashirika ya dini.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More