Tuesday, May 22, 2012

Serikali inasita nini kutumia Kiswahili kufundishia shule za sekondari? 



Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Elizabeth Missokia (aliyesimama katikati) akizungumza katika uzinduzi wa kitabu cha Kemia kilichoandikwa kwa lugha ya Kiswahili na Kingereza 'Furahiya Kemia'
Na Fredy Azzah - Mwananchi

MJADALA wa lugha gani itumike kufundishia katika shule za sekondari na hata vyuoni, umedumu kwa muda mrefu sasa nchini bila ya kuwapo ufumbuzi mwafaka.


Hata hivyo, watetezi wa Kiswahili wakiwamo  na watunzi wa vitabu wanaendelea na juhudi zao kuthibitisha kuwa lugha hiyo ina uwezo mkubwa wa kutumika kama lugha ya kufundishia shuleni na hata vyuoni.

Mfano mzuri wa juhudi hizo ni uandishi wa kitabu cha somo la Kemia kilichoandikwa kwa lugha ya Kiswahili kwa ajili ya kutumika katika shule za sekondari nchini.

“Tukiendelea kukishikilia Kiingereza, hatutatoka hapa asilani. Mbona wenzetu wa Ufaransa, Ujerumani na China wanatumia lugha zao?” anasema  Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya uchapishaji vitabu ya Mkuki na Nyota, Walter Bgoya katika  uzinduzi wa kitabu hicho hivi karibuni.

Anaeleza kuwa  kitabu hicho kiitwacho “Furahia Kemia”, kimeandikwa na jopo la walimu na kimelenga kujibu hoja ya watu wanaodai kuwa Kiswahili hakiwezi kutumika kufundishia shule za sekondari.




"Hiki ni kitabu cha kwanza tu kuandikwa, lengo letu ni kuandika vitabu vya masomo yote ya sayansi kwa lugha ya Kiswahili," anaongeza kusema.

Hata hivyo,  anasema kitabu hicho pia kimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza kwa kuwa bado mtalaa wa elimu ya sekondari nchini unaitambua lugha hiyo kama lugha ya kufundishia.
Kwa mujibu wa Bgoya, uandishi wa kitabu hicho kwa lugha zote mbili siyo tu  unaweza kumrahisishia msomaji, lakini pia  unamwezesha mwanafunzi kujifunza lugha       hizo.

"Ni kweli kuwa lugha ya Kiingereza ni tatizo kwa watoto wetu, badala ya kujifunza dhana ya Kemia ama somo jingine, utakuta wanajifunza lugha na ndiyo maana akisoma kidogo, hutafuta kamusi ya Kiswahili ili imsaidie," anabainisha na kuongeza:
"Kamusi hizi wanazotumia ni za lugha siyo za Kemia, kwa hiyo mtoto anashindwa kupata dhana  anayoitafuta.  Lakini kwa kutumia kitabu hiki, kitamwezesha kujua kila kitu kwa ufasaha."

Bgoya anasema licha ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kukikataa kitabu hicho kwa kuwa kimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili, tayari kimeshapata baraka na kukubaliwa na wataalamu wa Kemia nchini, Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita)  na Taasisi ya Elimu Tanzania Nchini (TET).
"Wangesema kina upungufu wa kitaalamu tungekibadilisha, lakini wamekikataa tu kwa sababu eti kimeandikwa katika Kiswahili. Tatizo la Taifa hili ni viongozi wetu wa elimu, lugha ni daraja tu la kufikisha maarifa, hivyo Kiswahili kikitumika watoto watayapata vizuri sana maarifa kwa sababu ni lugha wanayoifahamu,"anafafanua.

Kwa upande wake, mtunzi mashuhuri wa vitabu na mwalimu mstaafu wa somo hilo, William Mkufya anasema vitabu vya aina hiyo vitasaidia kuinua kiwango cha wanafunzi kuelewa masomo ya sayansi na kuwasaidia kuwa wabunifu.
Mkufya aliyewahi kufundisha katika shule za sekondari za Mzumbe na Zanaki, anasema mbali na kitabu hicho kuwafundisha watoto dhana za sayansi kwa kutumia lugha mama yao, pia kitawasaidia kujua lugha za  Kiingereza na Kiswahili kwa pamoja.

“Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imekuwa na kigugumizi cha muda mrefu  kubadilisha mfumo wa elimu na lugha ya Kiswahili kutumika kuwafundisha watoto, lakini hali halisi  tunaiona shuleni jinsi watoto wanavyoteseka,” anasema na kuongeza:
“Hata mwalimu akifundisha kwa Kiingereza ili mtoto aelewe, inabidi afafanue kwa Kiswahili. Mtoto naye anasoma kwa Kiingereza, lakini anakimbilia kamusi ya Kingereza na Kiswahili ili kupata maana. Hata hivyo, hizi kamusi ni za lugha siyo Kemia, kwa hiyo watoto wanapotoka zaidi.”

Aidha, anasema faida nyingine kubwa ya kitabu hicho ni kuwafanya wanafuzi kuwa wabunifu kwa sababu kimeeleza jinsi ya kutengeneza vifaa vya  majaribio ya Kemia  kwa kutumia vifaa vilivyo kwenye mazingira wanamoishi, badala ya kutegemea majaribio ya kwenye maabara ambazo hata hivyo hazipo katika shule nyingi nchini.
Mkurugenzi wa shirika la HakiElimu, Elizabeth Missokia, anasema kuandikwa kwa kitabu hicho ni moja ya ubunifu wa hali ya juu kwa kuwa kimeandikwa na jopo la walimu wa Kitanzania na kwa kutumia lugha wanayoifahamu wanafunzi.
“Unapomfundisha mtoto somo lolote kwa lugha mama, anaelewa vizuri zaidi kuliko kutumia Kiingereza. Hapa kwetu wote ni mashahidi kuwa wanafunzi wanapokwenda shuleni hutumia muda mwingi kujifunza Kiingereza na wakifika kidato cha tatu ndio wanaanza kujifunza dhana za masomo,” anasema na kuongeza:

“Itakuwa ni vizuri sana kama Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, itaona kuwa huu ni ubunifu na ianze kuufanyia kazi, kwani ni jambo litakalowasaidia watoto wetu.’’
Naye Mchunguzi wa Lugha kutoka Baraza la Kiswahili, Gertrude Joseph anasema asilani kamusi za lugha haziwezi kuwasaidia wanafunzi kujifunza dhana za masomo wanayosoma, hivyo anawahimiza walimu kuandika vitabu  kwa lugha ya Kiswahili ili viwasaidie watoto kuelewa  wanachojifunza.

“Sisi Bakita tunataka Kiswahili kifundishwe kuanzia mwanzo mpaka mwisho, kama kweli tunataka watoto wetu waelewe kile wanachofundishwa. Lugha yetu ndiyo itawasaidia watoto wetu kuwa wabunifu na wagunduzi,”  anaeleza.
Kwa upande wake, mwalimu Euniesta Saru anasema kwa muda mrefu amekuwa akipata tabu kufundisha somo hilo kwa kutumia lugha ya Kiingereza ambayo wanafunzi hawaielewi barabara.

“Wanafunzi wanaotoka shule za mchepuo wa Kiingereza ni afadhali, lakini kwa wanaotoka  shule za kawaida kweli wanapata shida. Ni  vema hivi vitabu vikasambazwa katika shule zote ili vitusaidie walimu na hata wanafunzi,” anasema mwalimu huyo.

Pamoja na kukubali kutokuwapo kwa athari ya kitabu hicho kimatumizi, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) inasema haiwezi kukitambua kitabu hicho kwa kuwa kimekataliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo ndiyo mamlaka pekee nchini inayotoa ithibati ya vitabu vya kutumika shuleni.
Aidha,  TET yenye jukumu la kuandika na kusimamia mitalaa nchini inasema kuandika kitabu hicho kwa kutumia lugha ya Kiswahili, ni kuvunja utaratibu kwa kuwa mfumo wa elimu ya sekondari unakitambua Kiingereza kuwa lugha ya kufundishia.

“Athari ya moja kwa moja kwenye mitalaa siwezi kusema kama ipo, lakini ninachokiona ni kuvunja utaratibu uliowekwa kwa kuwa lugha ya kufundisha ni Kiingereza,” anasema ofisa wa TET, Habib Fentu.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More