Thursday, March 29, 2012

Pinda ataka wadau wa elimu kutafuta muarobaini wa changamoto za elimu Tanzania


Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda akizungumza
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewataka washiriki wa mkutano wa taifa juu ya maendeleo ya elimu nchini kutafuta njia bora ya ufumbuzi wa changamoto zinazochangia kudhoofisha maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
Waziri Pinda ametoa kauli hiyo katika ufunguzi wa mkutano huo wa taifa wa elimu ulioandaliwa na Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kuinua kiwango cha elimu nchini.
Kuhusu elimu ya awali, amesema kuwa watanzania wengi hususani wa vijijini wamekuwa hawaipi kipaumbele kiasi kwamba watoto wakipelekwa shule za msingi wanacheza kwa sababu wamekosa fursa ya kucheza katika shule za awali. Amesisitiza kuwa kila shule ya msingi iwe na darasa la awali ili kuwafanya watoto kuzoea mazingira ili wanapoanza shule ya msingi waanze kukabiliana vizuri na masomo.
Akizungumzia suala la mikopo kwa elimu ya juu, Pinda amesema serikali ilianzisha hilo kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi ambao wanakwenda kujiendeleza katika masomo hayo lakini hivi sasa imebaini kuwa kuna changamoto kubwa serikalini kwani fedha hazitoshi kutokana na wanafunzi kuwa wengi. Amewataka wadau hao kuja na mbinu mpya ya kuweza kutoa mikopo kwani wanafunzi hao wamekuwa hawarejeshi mikopo yao hali inayoipa serikali wakati mgumu.
Naye Mkuu wa Shule hiyo ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Professa Alistella Balalulisa amesema kuwa wameamua kufanya mkutano huo kutokana na taaluma ya elimu inavyokwenda hapa nchini ikizingatiwa kwamba kiwango cha ufaulu katika shule za msingi na shule za sekondari kimekuwa kikishuka mwaka hadi mwaka na kulalamikiwa na wadau mbalimbali wakiwemo wazazi ambao wanaitupia lawama sekta ya elimu nchini.
Amesema wao kama wanataaluma wameamua kuitisha mkutano huo ili kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo na kutoa njia ama mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo. Mkutano huo wa siku tatu umewakutanisha wadau mbalimbali wa elimu nchini ambao ni watafiti na walimu wanaofundisha katika sekta mbalimbali za elimu hapa nchini.

Habari na picha kwa mujibu wa mtandao wa Thehabari.com
Short URL: http://www.thehabari.com/?p=14978

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More