Wednesday, March 21, 2012

CLUB ZAOMBA MAKTABA, TUISHENI KUNUSURU UFAULU KIDATO CHA IV, 2012


Wanachama wa Club za Marafiki wa Elimu Dodoma kutoka katika shule mbalimbali Mkoani Dodoma wameomba msaada wa kupata walimu na Maktaba za jamii ili kuwanusuru na matokeo mabaya katika mtihani wa kidato cha nne na kidato cha pili mwaka huu.
Wanachama hao ambao ni wanafunzi wa shule za sekondari kutoka katika shule mbalimbali ndani ya Manispaa ya Dodoma wamesema ili kuhakikisha kuwa wanachama wa Club hizo wanakuwa mfano wa kuigwa katika matokeo yao ni vyema uwepo mkakati wa aina yake wa kuongeza ufaulu kwa kuwapatia wanachama hao masomo ya ziada na fursa ya huduma za Maktaba ili kuongeza ufaulu wao.
Maombi hayo ya wana Club yamekuja kufuatia uchambuzi uliofanywa na wanachama hao kwa ushirikiano na MED kuhusu kero ambazo zinawafanya wasifanye vizuri kwenye mitihani yao ya kidato cha pili na ile ya kidato cha nne.
Wakiongea katika mjadala huo wanafunzi hao wamekiri kuwa juhudi za ziada za kila mwanafunzi zinachangia kwa zaidi ya asilimia 70% kiwango cha 30% kilichosalia kinapaswa kutoka kwa walimu, jamii, wazazi na wadau wengine. "tunajitahidi lakini wadau wengine nao watusaidie kupata vitabu na walimu kwa masomo ya ziada ili tufaulu" alisema Charles Chunga pichani mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Kikuyu Sekondari.
Wakiunga mkono wazo hilo wanafunzi hao walitoa ombi kwa wadau kuchangia uanzishwaji wa Maktaba za jamii na kutafuta namna ya kuwezesha walimu wa masomo ya ziada ili wanafunzi wasio na uwezo wa kujiunga na Maktaba ya Mkoa na malipo makubwa ya tuisheni wapate huduma hiyo kwa gharama nafuu au bure kabisa pale inapo wezekana.

Imeandikwa na Davis Makundi wa Marafiki wa Elimu Dodoma (MED)

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More