Sunday, November 13, 2011

Wabunge wapinga sera mpya ya elimu

Wanafunzi wa shule ya msingi Mwisenge iliyopo wilayani Musoma katika matukio mbalimbali shuleni hapo



WABUNGE wameponda rasimu ya Sera ya Elimu na kusema haina lolote jipya zaidi ya kuendeleza machungu kwa Watanzania.Katika michango yao, wabunge hao walisema sera hiyo inakuja wakati Watanzania wengi wanaendelea na machungu ya kueleza hisia zao na kwamba, kila kona ya nchi kumekuwa na malalamiko ya mfumo mzima wa elimu, jambo linaonyesha mambo hayaendi vizuri.

Akiwasilisha rasimu ya sera hiyo, Mchambuzi wa Sera Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Calistus Chonya, alisema inaruhusu wanafunzi waliopata mimba kurudishwa shuleni.Chonya alisema ndani ya sera hiyo, elimu ya sayansi ya jamii itakuwa ya lazima, wanafunzi kuanza masomo ya shule ya msingi wakiwa na umri wa miaka sita na elimu ya msingi mwisho utakuwa darasa la sita.

Pia, kuwapo ulazima wa wanafunzi kujifunza masomo ya ufundi shule za elimu ya juu na kingine ni watoto wa shule za awali kutokaa bweni.Katika michango ya wabunge, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) Stephen Wasira, alisema sera hiyo inalenga kuwapotosha wananchi na haina jipya lolote ndani yake, kwani inaleta machungu.

“Mwenyekiti, hapa ni kama tunadanganyana hakuna kitu chochoe na hakitakuwapo, hivi mtoto mdogo asome mwisho darasa la sita na anamaliza akiwa na umri wa miaka 12 hivi anakwenda kufanya nini kwa mama yake?’’ alihoji Wasira.Wasira alitaka wizara hiyo kufikiria jinsi ya kuongeza miaka ya idadi ya madarasa wanayotakiwa kusoma wanafunzi, ili angalau watoto wasome hadi madarasa ya juu kuliko kama inavyopendekezwa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Longido, Michael Laizer, alitaka wizara kufuta kabisa mpango huo, kwani hauna jipya ambalo linaweza kuwa nuru kwa Watanzania zaidi ya kuongeza machungu.Laizer alitaka wizara kufikiria kwanza kumaliza ubaguzi uliopo ndani ya ofisi na idara zake kuliko kuanza kutunga sera zingine ambazo alieleza kuwa, zilikuwapo bali utekelezaji wake ni mbovu.

“Kuna ubaguzi mkubwa ndani ya wizara yenu halafu mnakuja na jambo jingine, kwanza hii wizara itoke Tamisemi maana huko limekuwa dudu kubwa ambalo halina mpango wowote,” alisema Laizer.Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida Mbunge wa Nkenge, Asumpta Mshama, alipinga utaratibu wa wanafunzi kurudishwa shuleni wakiwa na mimba.

“Mwenyekiti, haiwezekani! Ni aibu kubwa kumrudisha mwanafunzi aliyepata mimba shuleni, hiyo ni aibu wasirudishwe kabisa mimi napinga,’’ alisema Mshama.

Wakiwasilisha sera hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizaya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Selestin Gesimba, alikiri kuwapo manung’uniko makubwa katika wizara hiyo yanayotokana na utaratibu unaotumika sasa.

Habari hii imetoka gazeti la Mwananchi na imeandikwa na
Habel Chidawali, Dodoma



0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More