Thursday, November 17, 2011

TAMKO KUHUSU UWAZI KATIKA BAJETI, UWAJIBIKAJI NA USHIRIKISHWAJI





TAMKO LA DAR ES SALAAM KUHUSU UWAZI KATIKA BAJETI, UWAJIBIKAJI NA USHIRIKISHWAJI

Sisi ni nani

Sisi ni raia na asasi za kiraia kutoka kote duniani, ambao tumeunganishwa na imani kwamba uwazi na ushirikishwaji katika bajeti za umma ni muhimu sana katika kujenga dunia ambayo binadamu wote wanafurahia haki zao za binadamu- kiraia, kisiasa, kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kimazingira.

Kwa kipindi cha miaka kumi na tano iliyopita tumejifunza, tumefanya kazi na kupambana ili kufanya bajeti na michakato ya bajeti kuwa ya wazi zaidi na shirikishi katika ngazi zote za serikali. Tumeonesha kwamba ushiriki wa asasi za kiraia unaweza kuboresha kwa kiwango kikubwa michakato ya bajeti, maamuzi na matokeo, na hatimaye kubadili maisha ya watu.

Tunu za harakati zetu za kimataifa

Bajeti za umma hupatikana kupitia michango ya wananchi na kipato kinachotokana na rasilimali za umma. Kwa maana hiyo, msingi wa imani wa harakati zetu ni kwamba ushiriki katika maamuzi yanayohusu bajeti za umma ni haki ya msingi na wajibu wa wananchi wote.

Tumejitolea kwa dhati kuleta usawa wa kijamii na kwa kuwawezesha waliotengwa kabisa, kwa kukuza ushirikishwaji na usawa kama miongozo ya shughuli zetu zote.

Tunajitolea katika kuheshimiana na kutokubaguana, tukihakikisha kuwa hatutafanya utofautishaji kwa misingi ya kitabaka, ukabila, jinsia, rangi, dini au ubaguzi wa aina yoyote ile.

Tunatambua wazi uzoefu wetu wa pamoja na kusherehekea wingi wetu na utayari wetu wa kuchochea na kuunga mkono jitihada zinazoujenga uzoefu huu katika namna ambayo ni sahihi zaidi kwa kila maudhui.

Tunathamini na kukuza ushirikiano na wote waliojiunga pamoja kwa ajili ya lengo letu kupitia harakati zetu.

Tunaapa kuzingatia viwango vya juu vya uadilifu kwa harakati zetu na kutamka kutofungamana kwetu na vyama vya siasa, serikali, mashirika ya serikali za kimataifa, vyombo vya habari na sekta ya biashara.

Tunaamini kwa dhati kuwa huu ndio muda wa kuendeleza uwajibikaji, ushirikishwaji na uwazi wa bajeti za umma kote ulimwenguni. Katika kufanikisha mabadiliko haya, tunaunganishwa na dira, kanuni za pamoja, madai ya wazi na ajenda ya utekelezaji.

Dunia tunayoitaka

Mara nyingi imekuwa kwamba wananchi, na hasa wale waliotengwa, hawashirikishwi katika michakato ya mipango ya bajeti za umma. Ni muhimu na inawezekana kuondokana na dhana ya sasa, kwa kuzingatia misingi ifuatayo:

- Bajeti za umma lazima ziwe wazi, hii inamaanisha kwamba taarifa zote zinazohusu namna ambavyo fedha za umma zinavyokusanywa, kutengwa, kutumika lazima zipatikane kwa jamii nzima kwa urahisi, kwa wakati muafaka na namna ambayo inaeleweka.

- Michakato ya bajeti lazima iwe shirikishi, inayohakikisha kuwa kuna uwazi na fursa kubwa kwa wananchi wote kutimiza haki yao ya kujua, kushiriki na kushawishi maamuzi yote kuhusu ukusanyaji, utengaji na usimamizi wa fedha za umma.

- Bajeti lazima ipangwe na kutumika kwa ufanisi, kikamilifu na kwa usawa na lazima ihakikishe kwamba rasilimali za umma zinafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuondoa umaskini na kufanikisha usawa.

- Taarifa za bajeti lazima ziwe sahihi, zilizojikita katika makadirio yanayojulikana kwa jamii na kuhakikisha kwamba serikali inatumia pesa za umma kwenye vipaumbele vilivyopitishwa, hivyo basi kupunguza uwezekano wa upotevu, rushwa na kukosekana kwa ufanisi.

- Bajeti zinapaswa kuwa na maelezo ya kina, zikihusisha mapato yote na matumizi, bila kujali vyanzo vyake—ikiwemo misaada ya kimataifa, fedha za mashirika ya umma na usimamizi wa madeni ya ndani na nje.

- Bajeti lazima ziwe endelevu, kuhakikisha kwamba fedha za umma zinatekeleza malengo yote kwa kipindi cha muda mrefu, kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.

- Bajeti zinapaswa kuripotiwa mara kwa mara na kwa mfululizo katika ngazi zote za serikali.

- Bajeti lazima ziwe kitu cha ufuatiliaji wa kudumu, usimamizi na uwajibikaji wa wabunge, taasisi za ukaguzi za ndani na nje ya nchi, vyombo vya habari na wananchi.

Wito kwa:

Serikali zote katika ngazi ya kitaifa na serikali za mitaa:

  1. Zitambue, zitunge sheria, kupitisha sheria na kutekeleza haki ya kupata taarifa kwa ujumla na hasa taarifa za bajeti za umma;

2. Kushirikisha wananchi na washika dau wote katika kupanga vipaumbele vya bajeti—zikiwemo fedha za mashirika ya umma, pesa za kodi—mapema na kwa ushirikiswaji kadri inavyowezekana.

3. Kutengeneza na kujadili waziwazi, katika muda muafaka, angalau nyaraka nane muhimu za bajeti: taarifa kabla ya bajeti, makadirio ya bajeti, bajeti iliyopitishwa, bajeti ya wananchi, ripoti ya ndani ya mwaka, ripoti ya nusu mwaka ya utekelezaji, ripoti ya mwisho wa mwaka na taarifa za ukaguzi;

4. Kuripoti juu ya mtiririko wote wa fedha za umma na taasisi, zikiwemo zile ambazo husimamiwa nje ya mchakato rasmi wa bajeti;

5. Kuhusisha rasilimali zote zilizotumika katika utekelezaji wa sera za umma, sera za kifedha na sera za kiuchumi, bila kujali vyanzo vyake, katika nyaraka zote za bajeti ya umma na michakato yake;

6. Kuhakikisha kuwa wabunge na wakaguzi hawafungamani na serikali na wana rasilimali za kutosha kuongeza uwezo wao na hivyo kutekeleza jukumu lao la kusimamia kwa ufanisi.

  1. Kuchapisha na kusambaza taarifa za bajeti katika mfumo rahisi na unaofikiwa kwa njia zote zinazowezekana, ikiwemo mfumo wa taarifa wa wazi katika mtandao wa kompyuta, maktaba za jamii, vituo vya habari n.k

Wabunge wanapaswa:

  1. Kuongeza uwezo wao kutekeleza majukumu yao ya kikatiba kama wawakilishi wa mahitaji watu kwanza, na si matakwa ya serikali ama yao.
  2. Kuchukua kila hatua ya lazima ya kuleta ushiriki wenye maana na jumuishi wa wananchi katika mchakato wa kupanga bajeti za umma na hatua za utekelezaji, kupitia mikutano ya hadhara na mawasilisho.
  3. Kuziwajibisha serikali kwa kukusanya mapato ya umma na kutumia mapato ya umma ipasavyo au isivyopasa.

Taasisi za Ukaguzi za Umma zinapaswa:

  1. Kuongeza uwezo wao katika kutekeleza majukumu yao ya uangalizi ili kuifanya serikali iwajibike katika matumizi ya rasilimali za umma.
  2. Kufanya kazi bega kwa bega na asasi za kiraia kufanya ukaguzi wa huduma za jamii;
  3. Kufanya kazi kwa ukaribu na asasi za kiraia na wabunge kubuni kanuni za matumizi ya fedha za umma, kujumuisha fedha za mashirika ya umma na fedha za kodi, kubainisha vizuri, kukemea na kutafuta suluhisho la matumizi mabaya ya fedha za umma;
  4. Kuikagua serikali kwa uhuru kamili na kuiwajibisha serikali kwa kukusanya na kutumia fedha za umma kwa kuzingatia bajeti ya umma iliyopitishwa;
  5. Kufikia kwa mapana zaidi katika uwajibikaji kwa fedha zote za umma, zikiwemo fedha za taasisi ambazo ziko nje ya bajeti, ili kutambua wajibu wao katika msingi ya uwajibikaji.

Vyombo vya habari vinapaswa:

  1. Kutekeleza wajibu wake kwa maslahi ya umma, kwa kuhakikisha kuwa taarifa sahihi kuhusu bajeti za umma zinaeleweka na kusambazwa kwa kiasi kikubwa;
  2. Kufuatilia na kuripoti hadharani tukio lolote la matumizi mabaya ya fedha za umma;
  3. Kuripoti matukio ambapo asasi za kiraia na wananchi wanachangia kuboresha usimamizi wa fedha za umma;
  4. Kushirikiana na asasi za kiraia na wananchi kwa kuwapa nafasi ya kusambaza na kujadili matokeo yao ya ufuatiliaji wa bajeti.

Taasisi za Kimataifa za Kiserikali na wafadhili:

  1. Kusaidia ushiriki mpana na wa kina wa wananchi na wadau wengine katika masuala ya bajeti za umma;
  2. Kusisitiza jukumu kubwa la serikali la kuwajibika kwa wananchi wake; Kushirikiana na kuziwezesha serikali kuboresha uandaaji na utoaji kwa muda muafaka wa taarifa za bajeti za umma, kuanzisha michakato ya ushiriki na kufikia viwango vya juu kabisa vya uwajibikaji;
  3. Kushirikiana na kusaidia wabunge na taasisi za ukaguzi kuboresha uwezo wao wa kutekeleza majukumu ya usimamizi, kuandaa na kutoa taarifa sahihi za bajeti kwa muda muafaka zinazoweza kuiwajibisha serikali;
  4. Kutoa kwa serikali kwa wakati muafaka taarifa sahihi na za kina kuhusu mtiririko wa misaada ya nje ambayo wanatoa, katika mifumo ambayo inaendana na mifumo na michakato ya bajeti za serikali;
  5. Kuboresha taratibu zao ili kuleta uwazi na uwajibikaji wao na wa serikali kwa wananchi.

Wawakilishi wa wananchi na asasi za kiraia wanapaswa:

  1. Kuhusisha tafiti za bajeti za umma, ufuatiliaji na utetezi katika juhudi zao za kuleta haki ya kijamii na haki za binadamu;
  2. Kudai serikali na wabunge taarifa kuhusu bajeti za umma na kujielimisha wenyewe kuhusu masuala ya bajeti;
  3. Kuidhinisha na kudai haki yao ya kushiriki katika michakato ya bajeti;
  4. Kutumia sheria za upatikanaji wa taarifa kama zipo au kudai upitishwaji wa sheria hizi iwapo hazipo;
  5. Kujiunga na harakati zetu

Tunatoa wito kwa serikali zote na wadau katika sekta zote kufanyakazi pamoja, kuanzisha na kurasimisha desturi za kimataifa ili kuleta taratibu za bajeti za umma zenye uwajibikaji, ushirikishwaji na uwazi katika kuhakikisha upatikanaji wa haki za binadamu duniani kote.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More