Saturday, November 26, 2011

Prof Mosha: Sitasherehekea Miaka 50 baada ya Uhuru kwa haya katika Elimu


Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof Herme Mosha akionesha kitabu cha serikali cha Best.
Mi sitasherehekea miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika kwa kuona wanafunzi wanaendelea kukaa chini bila madawati ya kutosha kwani hakuna sababu ya kukaa chini na inawezekana wakakaa kwenye madawati kama serikali itaamua kufanya hivyo.
Pili ni kuwa na madarasa yenye mjazano mkubwa wa wanafunzi, mara nyingine hata zaidi ya 100 darasa moja.
Tatu utekelezaji wa kiholela wa baadhi ya miradi, watu wanatengeneza matofari 50 kwa mfuko mmoja wa saruji.
Je fedha zote zinazowekezwa kwenye elimu zinatumika ipasavyo?
Jambo jingine ni kuhusu uongozi wa elimu, changamoto kubwa sana, viongozi wengi hawataki kuona wamefanya nini kwenye sekta ya elimu bali wanajiuliza wamepata nini katika sekta ya elimu, Maslahi binafsi yanatawala maslahi ya umma.
Pia Mwaka huu (2011) "sitashangaa kama hali itakua mbaya zaidi katika matokeo ya mtihani hasa baada ya kuwa wa kwanza kufanya mtihani katika mtaala mpya.hali yaweza kuwa mbaya zaidi, katika matokeo ya kidato cha nne".

Mkurugenzi wa HakiElimu, Elizabeth Missokia akifungua kongamano la Elimu katika ukumbi wa Yombo 4 wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Elizabeth Missokia akiipongeza serikali na pia kukumbusha changamoto zilizopo ili kuhakikisha elimu inaboreka zaidi Tanzania inapoanza safari ya miaka 50 ijayo.

Ifuatayo ni hotuba fupi ya ufunguziwa kongamano
Katika kutafakari Hali ya Elimu; miaka 50 tangu tupate uhuru, serikali imefanya juhudi za makusudi za kupanua sekta ya elimu na pia kuiboresha kwa kubuni na kutekeleza mipango mbalimbali hasa elimu ya msingi na sekondari.
· Wakati tunapata uhuru mwaka 1961, tulikuwa na shule za msingi 3,238 zilizokuwa na wanafunzi 486,470, mwaka huu tuna shule za msingi 16,001 na wanafunzi 8,363,386.
· Mwaka huo wa 1961, tulikua na shule za sekondari 41 na wanafunzi 11,832 mwaka huu tuna shule za sekondari 4,367 na wanafunzi 178,9547 nchi nzima, pia wakati nchi inapata uhuru tulikuwa na vyuo vya ualimu vitatu na leo hii tunavyo 103.
Haya ni mafanikio makubwa; ni wazi kuwa fursa za elimu kwa watoto wetu zimeongezeka!
· Mifano hai ya kuonesha kuwa serikali imekuwa ikipigania sekta hii muhimu ni mipango na mikakati kama UPE, MMEM, (elimu ya msingi), MMES (elimu ya sekondari), MMEJU (elimu ya juu), MEMKWA (elimu ya msingi kwa walioikosa) ni dalili tosha ya kuwapo kwa dhamira ya dhati ya kuinua elimu nchini.
· Jitihada kubwa na pengine ya kihistoria ni mwaka 2005 serikali ilipobuni mkakati wa wananchi kujenga shule za sekondari kwenye kila kata, utaratibu ambao ulikuwa na sura ya kitaifa zaidi na kupigiwa debe vya kutosha na aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowasa ikiwa na lengo kuu moja ambalo ni kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata fursa ya kupata elimu ya sekondari.
o Mpango wa shule za kata uliongeza wanafunzi kwa kiasi kikubwa wanaojiunga na sekondari, mfano kwa mwaka 2001 wanafunzi wa sekondari walikua 289,699, mpaka kufikia mwaka huu 2011, shule za sekondari zilikua na wanafunzi 1,789,547 nchi nzima huku kukiwa na ongezeko la shule kutoka shule za sekondari 937 mwaka 2001 mpaka shule 4,367 mwaka 2011.
· HakiElimu inapongeza juhudi hizi, lakini pia changamoto zimebaki kuwa nyingi sana na pengine ndizo zinakwamisha juhudi za kuwapatia elimu watanzania.
o Baadhi ya changamoto sugu ni uhaba wa vitendea kazi kwa walimu, ukosefu wa maabara, maktaba, uhaba wa nyumba za walimu, vyumba vya madarasa pamoja na mazingira mabovu ya kujifunzia ambavyo vimechangia kuporomoka kwa elimu yetu
o Changamoto nyingine ni maslahi mabovu ya walimu na watumishi wa ngazi za kawaida mashuleni.
· Matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2010 ni kielelezo tosha cha kuporomoka kwa kiwango cha elimu nchini (nusu ya wanafunzi walipata daraja sifuri)!
· Je, tunaposherehekea miaka 50 ya uhuru, tunayatafakari haya?
· Ndugu zangu watanzania, tutafakari kwa kina sana mambo haya hasa kipindi hiki. Na tupange mikakati ya kutoka hapa tulipo.
· Bila shaka serikali sasa imetambua na kukubali kuwa hali ya elimu nchini si nzuri. Tunapaswa kushirikiana, na sio kuvunjana moyo kuboresha elimu yetu.
· HakiElimu kuanzia mwaka ujao, pamoja na mambo mengine tunafikiria kufanya tafiti za kutafuta majibu ya baadhi ya changamoto za elimu. Hatutaishia hapo. Tutaenda kushirikiana na jamii katika maeneo mbalimbali kutekeleza baadhi ya mapendekezo yanayotokana na tafiti zetu kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mwanafunzi aliyeko darasani ANAELIMIKA!
· Tunafarijika kwamba sasa watoto wetu tunao madarasani, tuendelee kuwaandikisha zaidi: lakini jambo la msingi: TUWAPE ELIMU BORA!
· Tunapoingia kwenye nusu ya pili ya karne hii kama Taifa, inatupasa tusirudie makosa. TULENGE KUANDIKA HISTORIA MPYA KATIKA KUBORESHA ELIMU YETU, AMBAPO VIZAZI VIJAVYO VITANUFAIKA NA JITIHADA ZETU

Wasikilizaji wakifuatilia mijadara mbalimbali

Meza kuu katika kongamano la kutathmini hali ya elimu nchini, Miaka 50 baada ya uhuru wa Tanganyika.Kutoka kushoto ni Prof Herme Mosha,Ayub Rioba,Dr Hillary Dachi na Dr Kitila Mkumbo wote wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More