Wednesday, April 6, 2011

HakiElimu yatahadharisha nchi juu ya wasomi bandia


Mkurugenzi wa HakiElimu Elizabeth Missokia akionesha ripoti ya utafiti juu ya uhusiano wa Ubora wa Mitaala na Utoaji Elimu Bora.Kulia ni Meneja wa Idara ya Habari Bwana Nyanda Shuli

Kutokana na utafiti uliofanywa na HakiElimu hivi karibuni na kuzinduliwa rasmi leo, HakiElimu imependekeza Kamati ya Uidhinishaji wa Vitabu vya Kiada (EMAC) ifanyiwe maboresho ili kulinisuru taifa dhidi ya jamii ya wasomi bandia.

Mapendekezo hayo yametokana na ukweli kwamba vitabu vingi vya kiada ambavyo vimepitishwa na kamati hiyo vina makosa ambayo yanawapotosha walimu na wanafunzi.

Mapendekezo hayo yametokana na utafiti uliofanywa na HakiElimu (2010) kutathmini ubora wa vitabu vya hisabati vya shule za msingi na kubaini kuwa na makosa mengi kwenye vitabu ambavyo vimeidhinishwa na EMAC. Mapendekezo hayo yanalenga kuiboresha kamati hiyo muhimu katika utoaji wa elimu nchini.

Hayo yalisemwa leo na Mchambuzi wa Sera wa HakiElimu Bwana Mtemi Zombwe wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti uliofanywa na HakiElimu kuhusu Uhusiano wa Ubora wa Mitaala na Utoaji Elimu Bora.mikoa iliyoshirikishwa kwenye utafiti ni Arusha,Iringa,Tanga,Mwanza,Tabora na Shinyanga.

"kama EMAC inapitisha vitabu vibovu nchi itakua na wasomi wabovu na hivyo kuwa na wasomi bandia ambao hawataweza kusukuma gurudumu la maendeleo nchini," alisema Mtemi Zombwe ambaye ni mtafiti wa sera katika Idara ya Sera na Utetezi, HakiElimu.

Bwana Zombwe pia alisema bila kuchukua hatua hiyo muhimu ya kuboresha EMAC nchi itaendelea kubaki maskini.

EMAC ndicho chombo kikuu cha kuhakikisha ubora wa vitabu vya kiada mashuleni nchini kote.


Mkurugenzi wa HakiElimu Elizabeth Missokia akiongea na waandishi wa Habari


Mtemi Zombwe akiwasilisha matokeo ya utafiti
Utafiti ukiwasilishwa


Wadau muhimu wa HakiElimu, Waandishi wa Habari

Picha zote na Mashasi Edwin

1 comments:

Napenda kuwapongeza HakiElimu kwa kuonesha jinsi gani mlivyo na nia ya dhati kuleta mabadiliko ya kweli katika sekta muhimu ya elimu hapa nchini kwetu. Utafiti mlio ufanya nakubaliana nao kwa asilimia kubwa. Wanasiasa nndio wanaoharibu nchi yetu, imefika hatua wamechakachua sekta ya elimu mpaka kufika leo hii wanafunzi anayemaliza shule hajui kusoma wala kuandika. kwa kumbukumbu zangu za nyuma aliyekuwa waziri wa elimu kipindi hicho Mungai ndiye alioharibu kwa kiasi kikubwa mtaala wa elimu yetu. Utekelezaji wa Mtaala mpya umekuwa na changamoto nyingi kiasi cha kuhataraisha ukuaji wa taifa let. kuna hatari mbele zinaonekana kuwa Tanzania itakuwa na vijana wengi ambao hawana uwezo, hawana maarifa, hawajui kusoma na kuandika. kwa hiyo taifa hili litakuwa la wajinga watupu. Naombeni utafiti huu muuchapishe japo kwenye magazeti ya kiswahili hili watanzania wajue mstakabali wa nchi yao.

ni mimi mdau wa Elimu mkoa wa Kagera

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More