Thursday, March 31, 2011

HakiElimu yazindua shindano la Insha, katuni

TAASISI ya HakiElimu imezindua shindano la kuandika Insha au kuchora katuni yenye kuelezea sifa anazostahili kuwa nazo mwanafunzi bora kwa ajili ya kukuza elimu nchini.

Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa, mwanafunzi ni daraja muhimu linalovusha makundi ya taaluma nyingine zote katika jamii kwa kuwa wanafunzi wa sasa ndiyo viongozi wa taifa katika siku zijazo.

Kaimu Mkurugenzi wa HakiElimu, Robert Mihayo alisema Dar es Salaam jana kuwa, lengo la shindano lenye kuhoji, ‘Je, mwanafunzi bora anapaswa kuwa na sifa gani muhimu’ ni kuwashirikisha wananchi na jamii katika jitihada za kuboresha elimu nchini na kuibua mjadala wa kitaifa juu ya njia za kuinua kiwango cha elimu.

Mihayo alisema shindano hilo ni la wazi kwa Watanzania wote wenye nia au dhamira ya kuona kunakuwa na mabadiliko chanya ya elimu ambapo washiriki 62 watapata zawadi zanye thamani ya Sh milioni 6.7.

“Katika zawadi hizo, mshindi wa kwanza na wa pili watazawadiwa shilingi 500,000 pamoja na redio moja kila mmoja, wengine 10 watakaofuatia watajishindia shilingi 200,000 na redio moja kila mmoja huku washindi wengine 50 watajishindia redio moja kila mmoja. Redio zinazotolewa kwa washindi ni zile zinazotumia nishati ya jua zenye thamani ya shilingi 60,000,” alifafanua Mihayo.

Alisema mwisho wa kutuma Insha hizo zisizozidi kurasa mbili ni Mei 30, mwaka huu na baada ya uchambuzi wa Insha na michoro, 12 zitakazoongoza kwa ubora zitatumika kutengeneza kitabu kitakachosambazwa nchi nzima ili kuwafikia wengi zaidi.

Mchambuzi katika taasisi hiyo, Mtemi Zombo alisema, tangu kuanza kwa taasisi hiyo, wamefanya mashindano saba katika mada mbalimbali ambapo mawazo ya wananchi hupelekwa kwenye sekta husika na matokeo yake yameonekana.

Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko
HabariLeo

1 comments:

Nataka kushiriki hili shindano kwa upande wa katuni lakini sijaona addres na vigezo na masharti ya shindano naomba kupata more information email yamgu ni cedgarjoel@yahoo.com

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More