Thursday, August 9, 2012

Uhaba wa Madarasa: Wanafunzi wa Darasa la Tatu Korogwe Wasomea Uchochoroni




Wanafunzi wa darasa la tatu shule ya msingi Silabu wakiwa darasani.
Darasa hili ni uchochoro uliopo shuleni hapo unaotenganisha jengo hadi jengo.

Wanafunzi wa darasa la tatu wa Shule ya Msingi Silabu wakitoa salamu 
kwa mwanahabari wa Thehabari.com alipowatembelea.

Picha juu na Chini ni Wanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Silabu
 wakiwa kwenye darasa lao.
Baadhi ya  walimu wa Shule ya Msingi Silabu, wakiwa kazini

 Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Silabu, Mizeki Charahani akiwa ofisini kwake.

 Na Joachim Mushi, Korogwe
WANAFUNZI wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Silabu iliyopo Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga wanasomea kwenye uchochoro unaotenganisha kati ya darasa moja na lingine kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Wanafunzi hao ambao darasa lao limekuwa likihama kila muda kutengemea hali ya hewa (jua na mvua) kufuata kivuli wamelazimika kusomea nje kwenye uchochoro ambao haujaezekwa kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni katika shule hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Silabu, Mizeki Charahani alisema wanafunzi hao wamelazimika kusomea nje kwa kuwa wanavyumba vinne tu vya madarasa ambavyo havitoshelezi kwa mahitaji ya shule.
Akifafanua zaidi alisema darasa hilo eneo lao maalumu la kusomea (darasa) ni kwenye uchochoro unaotenganisha kati ya darasa moja na lingine, lakini huwa wanahama jua linapozidi au mvua kunyesha na kwenda eneo lingine linalokuwa na kivuli.
“Darasa hili kwa kweli huwa linahama kulingana na hali ya hewa, jua likizidi wanabeba madawati yao na kuhamia eneo lenye kivuli, mvua ikinyesa hivyo hivyo wanahamia sehemu nyingine…lakini muda mwingine tunawahamishia kwenye darasa moja na wenzao pale kunapokuwa hakuna mwingiliano wa vipindi,” alisema Charahani.
Alisema shule hiyo yenye darasa la kwanza hadi la saba unauhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa kwani hata darasa la kwanza na la pili wanasomea kwenye darasa moja kwa kupokezana.
“Kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa hata hatuna darasa la awali wala ofisi ya walimu…na sisi ofisi yetu ipo hapa chini ya mti huu,” alisema Mwalimu huyo huku akionesha eneo moja chini ya mti ulio mbele ya madarasa ya shule hiyo.
Akizungumzia hali hiyo, Ofisa Elimu Taaluma, Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Elius Mkwizu alikiri kuwepo kwa tatizo hilo la uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo na kudai shule hiyo ni mpya hivyo ujenzi wake haukwenda sambamba na ongezeko la wanafunzi kimadarasa.
Alisema tayari uongozi wa idara hiyo kwa kushirikiana na wananchi unafanya ujenzi wa madarasa mawili ambayo yatasaidia kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo. Hata hivyo aliongeza ujenzi huo kwa sasa umesimama baada ya fedha zilizotengwa kurejeshwa hazina kuu baada ya kukaa kipindi kirefu bila kutumiwa.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia moja ya ujenzi wa darasa lililosimama baada ya kukosekana kwa fedha za kuliendeleaza. Akifafanua zaidi Mkwizu alisema kulikuwa na mvutano kati ya viongozi waliokuwawakisimamia ujenzi huo na wananchi hali iliozua mgogoro na ujenzi kusimama.

Habari hii imeandaliwa na gazeti tando la www.thehabari.com kwa ushirikiano na HakiElimu

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More